Wafahamu viongozi wa dunia ambao hawajahudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II

Wawakilishi kutoka Syria, Venezuela na Afghanistan hawakualikwa kwenye mazishi ya Malkia,

Muhtasari

•Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman, hatarajiwi kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth siku ya Jumatatu.

•Hakuna mwakilishi kutoka Urusi, Belarus, au  Myanmar ambaye amealikwa .

Image: BBC

Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman, hatarajiwi kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa Reuters, ikimnukuu afisa wa Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza.

Alitarajiwa kwenda huko baada ya kupokea mwaliko rasmi kutoka Uingereza.

Saudi Arabia itawakilishwa na Prince Turki al-Faisal, shirika hilo lilinukuu chanzo hicho kikisema. Prince Turki ni Waziri wa Mambo ya Nje na amekuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri tangu 2018. Alikuwa mjukuu wa Mfalme Fahad na ni sehemu ya kizazi kipya kilicholetwa mamlakani na Prince Mohammed.

Vyanzo vilivyonukuliwa na Reuters vilisema kuwa mabadiliko haya yalitoka upande wa Saudi.

Utata tayari umeibuka kuhusu mwaliko uliotolewa kwa mwana mfalme wa Saudi Arabia.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani uamuzi wa kumualika mwana wa mfalme ambaye sasa ndiye msimamizi wa Saudi Arabia.

Mwana mfalme huyo anayejulikana kwa jina la "MBS", alishutumiwa na idara za kijasusi za nchi za Magharibi kwa kuamuru kuuawa kwa mwanahabari mzaliwa wa Saudia Jamal Khashoggi mnamo 2018. Hata hivyo, alikanusha kuhusika na mauaji hayo.

Tangu kuuawa kwa Khashoggi, Mohammed bin Salman hajafika Uingereza, kwa mujibu wa mwandishi wa usalama wa BBC, Frank Gardner.

Ingawa Saudi Arabia inashutumiwa kwa kukiuka haki za binadamu, bado ni rafiki wa karibu wa Uingereza.

Ambao hawajaalikwa

Wawakilishi kutoka Syria, Venezuela na Afghanistan hawakualikwa kwenye mazishi ya Malkia, kulingana na ripota wa BBC James Landale.

Hii ina maana kwamba viongozi wa nchi hizi hawatakwenda London na hawawezi kutuma ujumbe.

Hii ni kwa sababu Uingereza haina uhusiano wa kidiplomasia na nchi zote hizi.

Hakuna mwakilishi kutoka Urusi, Belarus, au  Myanmar ambaye amealikwa  , anasema mwandishi wa BBC James Landale.

Uhusiano wa kidiplomasia baina ya Uingereza na Urusi ulivunjika, tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, na msemaji wa rais wa Urusi Vladimir Putin alisema wiki iliyopita kwamba  "hakuwa anafikiria uwezekano " wa kuhudhuria mazishi. 

Sehemu ya uvamizi wa Ukraine ulianzishwa kutoka eneo la Beralus, ambayo rais wake, Aleksandr Lukashenko, ana ushirika wa karibu na Rais Putin. 

Uingereza pia imeondoa kwa kiwango kikubwa uwepo wake wa kidiplomasia kutoka  Myanmar tangu yalipofanyika mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo mwezi Februari  2021.

Korea Kaskazini na Nicaragua zilialikwa kutuma mabalozi pekee, lakini hazikuruhusiwa kutuma viongozi wao.