Mwanamke adhulumiwa baada ya kushuka matatu Thika

Mwathiriwa alitishiwa kwa kisu kabla ya kupelekwa kwenye kichaka kilichokuwa karibu kubakwa.

Muhtasari

• Jamaa alifikishwa mahakamani kwa madai ya kubaka msichana mmoja katika kituo cha mabasi punde baada ya kushuka matatu.

Mwanamume huyo aliokolewa na maafisa wa polisi toka kwa wananchi waliochukua sheria mikononi mwao.


Kituo cha mabasi
Kituo cha mabasi
Image: MAKTABA

Ubakaji ni changamoto ya kimataifa ambayo inawakabili wanawake matabaka mbalimbali na wa kutoka wa rangi zote.

Kumekuwa na ongezeko la visa vya ubakaji nchini Kenya, haswa katika maeneo ya mijini yenye watu wengi.

Hivi majuzi mwanamume wa umri wa makamo alifikishwa mahakamani kwa madai ya kubaka msichana mmoja katika kituo cha mabasi punde baada ya kushuka matatu.

Kulingana na ripoti ya polisi,mwanamke huyo alishuka kutoka kwa matatu akiwa na rafiki yake kuelekea nyumbani mjini Thika. Akiwa njiani, walitengana na rafikiye huku kila mmoja akielekea nyumbani njia tofauti.

Baada ya kutembea kwa mita chache mwathiriwa alikutana na mwanaume asiyejua na walipopitana, mwanamume huyo akageuka na kumfuata nyuma, ambapo alimtishia kwa kisu na kumpeleka kwenye kichaka kilichokuwa karibu na kumbaka.

Mwathiriwa alienda nyumbani na kumsimulia rafikiye tukio hilo na  akachukua hatua ya kumpeleka katika hospitali iliyokuwa karibu.Wakiwa njiani kuelekea hospitalini, wanawake hao wawili walikutana na mshukiwa na wakapiga nduru ambapo wananchi wenye hamaki walijaribu kuchukua sheria mikononi mwao.

"Wakiwa njiani kuelekea hospitalini, walikutana na mshukiwa na kupiga kelele ambapo wananchi walianza kujongea kusikiliza. Umma ulimshushia kumpiga huku wakipata kisu kirefu chenye ncha kali kutoka kwake," ripoti ya polisi ilisema.

Mshukiwa alikimbizwa katika hospitali ya Thika level 5 kwa matibabu huku polisi wakiendela na uchunguzi.

Mwathiriwa alikimbizwa hospitalini ya Romkan ambako alitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani akiwa na hali nzuri.