Familia ya mvulana wa miaka miwili aliyefariki katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta alipokuwa akifanyiwa upasuaji wa kuondoa jembe la uma lililokuwa kwenye fuvu la kichwa chake inaomba msaada wa kifedha kwa ajili ya mazishi yake.
Nyanya wa mvulana huyo Asha Njeri alisema kuwa familia hiyo ni maskini na haiwezi kupata pesa za kugharamia bili ya hospitali pamoja na gharama za mazishi.
Njeri alikuwa ametembelea familia hiyo katika kijiji cha Ndula huko Thika Mashariki kabla ya msiba huo kutokea.
Alisema bintiye, Judy Muthoni, mama wa marehemu ni mama asiye na mwenzi na mfanyakazi wa kawaida katika kijiji hicho na kwa hivyo atakabiliwa na kazi kubwa ya kutafuta pesa zinazohitajika.
“Msiba huo umetusumbua sana, hasa binti yangu. Hawezi hata kuongea kwa sasa. Inauma sana. Tunaomba watu wenye nia njema watusaidie gharama ya kumlaza kijana wetu,” Bi Njeri alisema.
Njeri alisema yeye na Muthoni hawakuwa nyumbani ajali hiyo ilipotokea.
Marehemu na kaka yake mkubwa mwenye umri wa miaka mitano walikuwa wakicheza nje ya nyumba yao pamoja na watoto wengine wakati mtoto huyo alipopita mbele ya kaka yake aliyekuwa na jembe la uma na likatua kichwani kwa bahati mbaya.
"Hatukuwa nyumbani lakini bado tulikuwa ndani ya kijiji. Tulipigiwa simu na majirani wakitujulisha kuhusu ajali hiyo,” alisema.
Majirani, wakiongozwa na Rachael Harrison ambaye pia ni mfanyakazi wa kujitolea wa afya katika kijiji hicho, walisema kwamba walisikia kilio kikubwa cha mtoto huyo na kukimbilia eneo la tukio na kumkuta kijana huyo akivuja damu nyingi huku akiwa na jembe kichwani.
"Mvulana huyo alikimbizwa katika zahanati ya kijiji na daktari (aliyetambulika kama Cyrus) alimpa huduma ya kwanza na kisha kumkimbiza katika hospitali ya Thika Level 5 kwa gari lake," alisema.
Mvulana huyo alipofika hospitalini hali yake iliboreshwa na CT Scan kuchukuliwa kabla ya kuelekezwa katika KNH.
Hata hivyo, majirani hao walinyooshea kidole cha lawama wasimamizi wa KNH kwa kuchukua muda mrefu kumhudumia mvulana huyo, wakisema kuwa ni uzembe uliosababisha mvulana huyo asiye na hatia kufariki alipokuwa akifanyiwa upasuaji.
"Watu wana uchungu katika kijiji hiki na tunaamini kwamba maisha ya mvulana huyo yangeokolewa ikiwa angehudumiwa kwa dharura," Harrison alisema.
Hata hivyo, hospitali hiyo Jumanne katika taarifa yake ilisema mgonjwa huyo alikuwa amepoteza damu nyingi, na kwa sababu hiyo, utaratibu wa kuganda haungefanyika kama ilivyotarajiwa, na hivyo kuchelewesha upasuaji kwa kuwa hii ingekuwa hatari kwa mgonjwa.
“Mgonjwa huyo ametulizwa tangu wakati huo na kwa sasa anafanyiwa upasuaji katika thieta za KNH. Tunawahakikishia kuwa mtoto yuko chini ya uangalizi bora wa timu zetu,” hospitali hiyo ilisema.
Hospitali hiyo ilijibu tu baada ya Wakenya kuiwekea shinikizo kwenye mitandao ya kijamii.
Mnamo Jumatano, mwenyekiti wa hospitali hiyo George Ooko katika taarifa aliiondolea hospitali hiyo makosa au uzembe wowote.
"Mgonjwa alifika KNH saa sita unusu lakini hali na wakati wa jeraha bado haujabainika," alisema.
"Alipokelewa katika Idara ya Ajali na Dharura na timu yetu, ikiwa ni pamoja na madaktari bingwa wa upasuaji wa neva mara moja walianza matibabu na uchunguzi ili kubaini mbinu salama zaidi ya usimamizi."
Alisema uchunguzi wa kimatibabu na uchunguzi wa mgonjwa, ikiwa ni pamoja na CT Scans na kipimo cha damu ulithibitisha jeraha la kupenya kwenye ubongo.
"Hali ya mgonjwa iliendelea kuzorota licha ya kuingilia kati. Hata hivyo upungufu wa damu na kuganda kulikubalika ifikapo saa mbili asubuhi ya Oktoba 11, 2022 na uamuzi wa kuendelea na uondoaji wa kitu hicho cha kigeni ulifanywa,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema zaidi kwamba, "katika thieta, mgonjwa alipata matatizo na majaribio ya kufufua hayakufaulu. Kufuatia kifo hicho, wazazi hao walialikwa kwa mkutano wa familia ambapo mfuatano wa matukio ulijadiliwa na kuelezwa habari za kifo hicho.”
Uongozi wa hospitali hiyo ulitoa pole kwa familia kwa kifo cha ghafla cha kijana huyo.
“Uongozi wa hospitali unapenda kufikisha ujumbe wa rambirambi kwa wazazi na familia kwa msiba wao. Hili lilikuwa jeraha kubwa na la kusikitisha kwa mtoto wa miaka miwili,” Ooko alisema kwenye taarifa hiyo.
Wakati huo huo, polisi wa Thika Mashariki bado hawajaanza uchunguzi kuhusu kisa kilichosababisha mvulana huyo kujeruhiwa vibaya.
Mkuu wa polisi Lazarus Wambua, ambaye alizungumza kwa simu, alisema kuwa suala hilo bado halijaripotiwa kwa mamlaka, kwa hivyo wanalichukulia kama suala la kifamilia.
Wambua alisema kuwa taarifa walizopokea zinaonyesha kuwa mtoto huyo alikuwa akicheza na kakake mkubwa wa umri wa miaka mitano nyumbani kwao wakati mkasa huo ulipotokea.
“Mtoto huyo alipita mbele ya kaka yake mkubwa ambaye alikuwa ameshika uma wa kuchimba walipokuwa wakicheza. Kwa bahati mbaya, uma jembe ulitua kwenye kichwa cha mtoto huyo na ndivyo mkasa ulivyotokea. Hatuchunguzi suala hilo kwa sababu bado halijaripotiwa. Tunaelewa kuwa haikuwa makusudi,” alisema.
Utafsiri: Samuel Maina