Miguna Miguna: Safari ya wakili mwenye utata Kenya kuanzia kufurushwa hadi kurejea nchini

Miguna alilakiwa na umati mkubwa wa wafuasi na kuelezea furaha yake ya kurejea nyumbani baada ya takriban miaka mitano.

Muhtasari

• Tarehe 26 Machi 2018, Miguna alijaribu kurejea Kenya, Aliwasili katika Uwanja wa JKIA na alipotaka apewe nafasi ya kuingia kwa mujibu wa amri nyingi za mahakama, serikali ilikataa kumruhusu kuingia Kenya.

Mwanasiasa Miguna Miguna akiwa katika uwanja wa ndege wa JKIA katika picha ya awali
Mwanasiasa Miguna Miguna akiwa katika uwanja wa ndege wa JKIA katika picha ya awali
Image: EPA

Miguna Miguna, wakili Mkenya aliyefurushwa hadi nchini Canada mwaka wa 2018, amerejea nchini, akiwasili uwanja wa ndege wa JKIA mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi Alhamisi akiabiri ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Katika uwanja huo , Miguna alilakiwa na umati mkubwa wa wafuasi na kuelezea furaha yake ya kurejea nyumbani baada ya takriban miaka mitano akiwa ughaibuni.

“Ninashukuru sana kwa makaribisho mazuri ambayo mumenipa, na nina furaha sana kurudi nyumbani. Natanguliza shukrani zangu kwa Wakenya  wote ambao wamesimama nami," Miguna alisema.

Mwanasiasa huyo alifurushwa nchini Kenya na wapinzani wake wa kisiasa baada ya kudaiwa  kusimamia kiapo cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga muda mfupi baada ya upinzani kususia marudio ya uchaguzi wa mwaka 2017.

Huu hapa msururu wa matukio ya Miguna Miguna

 • 2007: Alikuwa kiungo wa timu ya kampeni ya chama cha upinzani nchi Kenya ODM wakati wa uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo aliteuliwa kuwa mshauri mkuu wa wakati huo Waziri Mkuu Raila Odinga kabla ya kudaiwa kuwa na  utovu wa nidhamu ambapo alisimamishwa kazi bila malipo. Adhabu hiyo iliondolewa baadaye lakini Miguna alikataa kurejea kuendelea na kazi yake.
 • Mwaka 2010, baadhi ya wanachama kutoka chama tawala cha PNU walimshtumu kwa kuwa raia wa kigeni  kwa madai ya kumiliki hati ya kusafiria ya Canada, kwasababu wakati huo sheria za Kenya hazikutambua uraia wa nchi mbili wakati alipopata uraia wa Canada. Hathivyo Miguna alihalalisha kitendo chake kwa kusema kwamba "Wakati mtu anapotoroka utawala wa kidikteta, mtu hutumia njia yoyote na hata Bw. Odinga aliwahi kutumia pasipoti ya Tanzania."
 • Mnamo 2012, alizindua kumbukumbu yake ya kwanza iliyoitwa Peeling Back the Mask: Quest for Justice in Kenya. Kitabu hicho kilimkosoa sana Raila Odinga na kuzua maandamano kutoka kwa wafuasi wa Odinga huko Ahero kaunti ya  Nyanza. Vilevile alishambuliwa alipokuwa akizindua kitabu hicho katika hoteli moja mjini Mombasa na kulazimika kuokolewa na polisi.
 • Mnamo 2016, Miguna alitangaza kuwa atawania nafasi ya Ugavana wa Nairobi kama mgombeaji huru. Alizindua manifesto ambayo iliahidi uongozi unaozingatia uadilifu, sera za mabadiliko zilizo wazi na za kimaendeleo, programu na dhamira ya utoaji huduma, uundaji wa ajira na maendeleo ya miundombinu. Hata hivyo alishika nafasi ya nne katika matokeo ya uchaguzi huo.
 • Mwaka 2017: Katika uchaguzi wa urais wa mwaka huu, kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga na wafuasi wake walidai kuwa ushindi wa Kenyatta katika uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu baada ya upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi huo mahakamani. Mahakama ya Juu ya Kenya ilibatilisha tangazo la Uhuru Kenyatta na William Ruto kuwa rais na Naibu Rais waliochaguliwa kihalali na kuamuru marudio ya uchaguzi uliosusiwa na upinzani ukisema uchaguzi huo usingeendeshwa kwa haki na kuaminika. Uhuru Kenyatta na William Ruto walitangazwa rais na makamu wa Rais mtawalia baada ya uchaguzi wa marudio.
 • Bado katika mwaka huohuo {2017} Katika mabadiliko makubwa ya mi simamo, yake Miguna, alikua mmoja wa watetezi wa Odinga waliozungumza zaidi baada ya uchaguzi wa urais wa 2017; pia aliibuka kuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa utawala wa Kenyatta, akiutuhumu kwa ubabe na kujiingiza madarakani.
 • Mwaka 2018, katika hafla ya kuapishwa kwa dhihaka, Miguna alimuapisha Raila Odinga, ambapo Odinga alijitangaza kuwa "rais wa watu". Serikali ilijibu kwa kuzima matangazo yote ya televisheni na redio na kuwakamata Miguna na wakili mwingine (T J Kajwang') ambao walikuwa wameshuhudia hafla hiyo .Miguna alifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka. Mahakama Kuu iliamuru Miguna aachiliwe kwa dhamana, lakini serikali ilikaidi maagizo hayo. Pasipoti ya Miguna ya Kenya ilichukuliwa na akafurushwe nchini .
 • Mnamo tarehe 26 Machi 2018, Miguna alijaribu kurejea Kenya. Aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kwa ndege kutoka Dubai, na alipotaka apewe nafasi ya kuingia kwa mujibu wa amri nyingi za mahakama, serikali ilikataa kumruhusu kuingia nchini. Alizuiliwa katika uwanja wa ndege kwa muda na kurudishwa kwa lazima Dubai ambako alikuwa ametoka.
 • Mnamo tarehe 28 Machi 2018, Human Rights Watch ilitoa taarifa ikitaka Miguna aachiliwe. Shirika hilo lilisema kwamba "Mamlaka za Kenya zinapaswa kutii kwa haraka amri nyingi za mahakama na kumwachilia au kumfikisha Miguna mahakamani."
 • Mnamo tarehe 14 Disemba 2018, mahakama kuu ya Kenya ilitoa hukumu ya kihistoria ambapo iliishtaki serikali kwa kukiuka kwa kiasi kikubwa haki za kikatiba na msingi za Miguna kama vile haki yake ya uraia wa kuzaliwa ambayo iliamua kwamba hakupoteza na serikali haiwez  kuisitisha. Mahakama pia ilisema kuwa Miguna alikuwa raia anayestahili kupata Pasipoti ya Kenya na kuamuru Serikali kumpa pasipoti mpya na halali.
 • Mnamo Desemba 2019, Miguna Miguna alitangaza hadharani nia yake ya kurejea Kenya kupitia akaunti yake ya Twitter ikiwa ni jaribio lake la tatu. Akitoa mfano wa ulinzi dhidi ya agizo la mahakama lililotolewa mnamo Desemba 2018 kumruhusu kurejea, alisema kuwa ndege yake ingetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi asubuhi ya tarehe 11 Januari 2020. Hata hivyo, kurudi kwake kulikatizwa wakati mashirika ya ndege ya Lufthansa na Air France yalipomkataza kuhudhuria safari zao za ndege zikitaja arifa nyekundu ambazo zilikuwa zimetolewa na serikali ya Kenya kuhusu safari yake iliyokusudiwa.
 • Mnamo Septemba,22 2022: Miguna alikuwa amesema awali ataondoka Canada Oktoba 25 na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) usiku wa Jumanne, Oktoba 25, 2022. Hata hivyo Ijumaa yake alitangaza mabadiliko, akisema sasa angewasili Kenya mnamo Oktoba 20, 2022 saa kumi na mbili asubuhi.

Kabla ya ndege yake kutua uwanja wa JKIA , Miguna alikuwa amewaarifu wafuasi wake kwamba amealikwa kwenye sherehe za Mashujaa, na baadaye ataungana na Rais William Ruto na Mkewe Rachel Ruto kwa karamu ya bustani katika Ikulu.