2022 imekuwa mwaka mkubwa kwa watu mashuhuri wapendanao. Baadhi wamefunga ndoa, baadhi wamechumbiana, wengine wamepata watoto, wengine wamerudiana na wengine pia kwa bahati mbaya wameachana au wametalikiana.
Kuna orodha kubwa ya watu mashuhuri ambao wamekatisha ndoa au mahusiano yao baada ya kutofautiana katika kipindi cha mwaka moja uliopita.
Katika makala haya tunaangazia baadhi ya watu mashuhuri ambao wametengana mwaka wa 2022:-
1. ARROW BWOY NA NADIA MUKAMI
Wanamuziki mashuhuri wa Kenya Arrow Bwoy na Nadia Mukami walithibitisha kwamba wanachumbiana mwaka jana na kubarikiwa na mtoto wao wa kwanza pamoja mwezi Machi mwaka huu.
Wiki chache zilizopita Nadia hata hivyo alithibitisha kutengana na mzazi huyo mwenzake baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Katika tangazo lake mapema mwezi Desemba, Nadia alibainisha kuwa yeye na Arrow Bwoy hawajakuwa pamoja kwa muda.
2. AKOTHEE NA NELLY OAKS
Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee alitangaza kuvunjika kwa mahusiano yake na aliyekuwa meneja wake Nelly Oaks takriban miezi sita iliyopita.
Wawili hao walikuwa wametengana miezi kadhaa kabla ya Akothee kuthibitisha kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii mnamo mwezi Juni.
Kwa sasa mama huyo wa watoto watano yupo kwenye mahusiano na mzungu Bw Omosh huku Nelly Oaks akidaiwa kufunga ndoa miezi michache iliyopita.
3. CORAZON KWAMBOKA NA FRANKIE JUSTGYMIT
Mwanasoshalaiti Corazon Kwamboka na mwekezaji wa mazoezi ya mwili Frankie JustGymIt walitengana mwezi Februari baada ya kuchumbiana kwa miezi kadhaa na hata kujaliwa watoto wawili pamoja.
Hata hivyo kumekuwa na madai kwamba wawili hao wameonekana pamoja mara kadhaa baada ya kutengana.
4. STIVO SIMPLE BWOY NA PRITTY VISHY
Mahusiano ya mwimbaji maarufu kutoka Kibra Stivo Simple Bwoy na mtumbuizaji Pritty Vishy yalikuja kujulikana mapema mwaka huu baada ya Vishy kuchapisha video iliyoonyesha wakifurahia muda pamoja chumbani mwake.
Wawili hao walitengana kati ya Machi na Mei huku Vishy akimshtumu Stivo kwa kumuacha na kujitosa kwenye mahusiano na mwanamke mwingine. Stivo pia aliibua madai mazito dhidi ya Vishy yakiwemo kutokuwa mwaminifu.
5. AMBER RAY NA IB KABBA
Mapema mwaka huu mwanasoshalaiti Amber Ray alikuwa akichumbiana na mcheza mpira wa vikapu wa Sierra Leonne IB Kabba kwa miezi michache kabla ya wawili hao kutengana hapo mwezi Aprili.
Amber Ray kwa sasa anachumbiana na Kennedy Rapudo huku Kabba bado akionekana kuwa na machungu.
6. HARMONIZE NA KAJALA
Ingawa sio Wakenya, wasanii wa Tanzania Harmonize na Frida Kajala Masanja wana ushawishi mkubwa sana nchini Kenya na mahusiano yao ya miezi michache yalifuatiliwa kwa karibu hata humu nchini .
Harmonize na Kajala walirudiana mwezi Mei mwaka huu baada ya kutengana kwa mara ya kwanza Aprili mwaka jana. Wawili hao hata hivyo walitengana miezi kadhaa baadae huku Kajala akithibitisha kusambaratika kwa mahusiano yao mapema mwezi huu.
7. ZARI HASSAN NA GK CHOPPA
Mapema mwaka huu, mwanasoshalaiti wa Uganda Zari Hassan alichumbiana na mfanyibiashara GK kwa miezi michache kabla ya kutengena mwezi Aprili.
Zari kwa sasa yuko kwenye mahusiano mengine na Shakib Cham Lutaaya na wawili hao hata wanapanga ndoa.