Kwa nini matumizi ya simu hayaruhusiwi wakati wa kupaa na kutua kwa ndege?

Matumizi ya vifaa hivyo inaruhusiwa mara tu ndege inapofikia urefu fulani.

Muhtasari

•Wahudumu wa ndege watakuomba uzime simu yako ya mkononi au uiweke kwenye 'flight mode' kabla ya kuondoka. 

•Ulimwenguni kote, ni mazoea kutotumia simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki huku ukiruka chini ya futi 10,000.

Image: BBC

Ikiwa uko kwenye ndege, wahudumu wa ndege watakuomba uzime simu yako ya mkononi au uiweke kwenye 'flight mode' kabla ya kuondoka. Abiria pia wanashauriwa kutotumia vifaa vingine vya kielektroniki kwenye ndege.

Lakini katika safari nyingi za ndege za kimataifa, matumizi ya vifaa hivyo inaruhusiwa mara tu ndege inapofikia urefu fulani. Baadhi ya waendeshaji wa ndege wametoa hata huduma ya Wi-Fi katika ndege. Je, unajua ni kwa nini simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki haviruhusiwi kutumika wakati wa kuruka na kutua kwa ndege?

Ajali ya mwaka 2006

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na BBC Future mwaka 2013, katika tukio la 2006, mfumo wa kuongoza ndege hiyo ulifanya kazi ipasavyo, ukionyesha tofauti ya hadi nyuzi 30 mara tu abiria alipozima DVD player aliyokuwa akitumia.

Baada ya mtu kuwasha kifaa, tatizo lile lilitokea tena, kulingana na ripoti iliyochapishwa katika Spectrum, kuchambua data 125 juu ya madhara ya vifaa vya elektroniki kwenye kuruka kwa ndege.

Ulimwenguni kote, ni mazoea kutotumia simu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki huku ukiruka chini ya futi 10,000.

Kwa nini matumizi ya simu za mkononi hayaruhusiwi katika ndege?

Kwa mujibu wa Devendra Pun, afisa mkuu wa kiufundi wa shirika la ndege la kitaifa la Nepal Airlines, kuna baadhi ya sababu za kivitendo za kutoruhusu matumizi ya simu za mkononi katika hali fulani wakati wa safari za ndege.

"Ndege inapofikia urefu fulani, kila kitu kikiwa kawaida, rubani anaruhusu kufungua sehemu ya kukaa na kwenda chooni, na katika hatua hiyo, simu za mkononi pia zinaweza kutumika," alisema. "Lakini haipaswi kutumiwa wakati wa kupaa na kutua."

Anasema si tu simu za mkononi bali pia masafa ya redio na masafa ya ultrasound yanaweza kuathiri vifaa uongozaji na vifaa vingine vya mawasiliano vinavyotumika kwenye ndege ambavyo pia huendeshwa na mifumo isiyotumia waya.

Kwa mujibu wa Pun, sababu kuu ni: Hatari ya kuingiliwa kwa masafa

"Wakati mwingine mawasiliano ya rubani yanaweza yasisikike au yanaweza kuathiriwa na kukwama kwenye masafa," alisema.

Achutananda Mishra, Msemaji Msaidizi wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Nepal, pia anasema kuwa kuna hatari kama hiyo. Kulingana naye, ndege inayoruka katika mwinuko wa chini inaweza kupata masafa ya simu za mkononi na wakati mwingine kuna hatari ya kuingiliwa na mawasiliano ya rubani.

"Ingawa masafa yanayotumiwa na ndege na simu ni tofauti, wakati mwingine kuna hatari ya kuingiliwa na ikitokea, mawasiliano ya ndege yanaweza kuathirika," alisema Mishra. Mara nyingi, mtandao wa simu hautaonekana hadi baada ya ndege kupaa na kutua.

Kwa nini hakuna mtandao wa simu kwenye ndege?

Image: BBC

Abiria aliyekuwa katika ndege ya Yeti Airlines iliyoanguka Pokhara hivi majuzi alikuwa anatikana mubashara kupitia mtandao wa Facebook. Wataalamu wanasema kwamba mitandao ya simu za mkononi inaweza kupatikana hadi urefu wa mita 40 hadi 60 juu ya mnara wa msingi wa simu.

"Unaweza kupata mtandao wa simu hata ndani ya ndege katika mwinuko wa chini," afisa mkuu wa shirika la ndege la Nepal anasema. Kulingana na yeye, ingawa baadhi ya ndege za kisasa zina vifaa vya Wi-Fi, matumizi yake pia huzimwa wakati wa kuruka na kutua.

Wakati wa kutua kwa ndege, rubani, wafanyakazi wengine na abiria pia wanapaswa kuwa waangalifu kwa sababu kunaweza kuwa katika hatari ya kuendesha kifaa chochote wakati huu.

"Sababu nyingine ya kutotumia hata vifaa vya matibabu wakati wa kutua ni kwamba ikiwa umakini wa abiria uko mahali pengine, wanaweza wasisikie maagizo yanayotolewa kwenye ndege," Pun aliongeza.

Simu inaweza kusababisha ajali?

Wataalamu wanasema kuwa kutumia simu au vifaa vingine vya kielektroniki hasa wakati wa kupaa na kutua kunahatarisha abiria na ndege.

"Tishio kwa ndege inamaanisha tishio kwa abiria. Jambo lingine ni kwamba usiposikiliza matangazo ndani ya ndege kwa kuwa makini na simu ya mkononi au vifaa vingine, wakati mwingine abiria wanaweza kujeruhiwa wakati kuna mtikisiko (mtetemeko) ndani ya ndege," anasema Pun wa Nepal Airlines.

Lakini Tume ya Ulaya hivi karibuni imetoa ruhusa kwa waendeshaji wa ndege kutoa teknolojia ya 5G na data ya simu ya kasi ya chini hata kwenye ndege.

Hii inamaaisha kwamba abiria wa ndege hawahitaji tena kuweka simu zao za mkononi katika 'flight mode' wakiwa angani na wanaweza kupiga simu au kutumia data ya simu wakati ndege inaruka. Walakini, bado haijabainika wazi jinsi mfumo huo utakavyotekelezwa.

"Kulikuwa na wasiwasi kwamba inaweza kuingilia mifumo ya kudhibiti ndege kiotomatiki," mtendaji mkuu wa Kamati ya Usalama wa Anga yenye makao yake nchini Uingereza Dai Whittingham aliiambia BBC hapo awali.

"Lakini uzoefu umeonyesha kwamba hatari ya kuingiliwa kama hiyo ni ndogo sana. Hata hivyo, inashauriwa kuweka simu ya mkononi katika flight mode kila wakati ukiwa kwenye ndege."