Uchunguzi: ‘Wagonjwa wa akili’ wazuiliwa kanisani kupata maombi ya uponaji

Watu wasio na hatia wamekuwa wakifungwa minyororo na kunyimwa chakula kama inavyostahili.

Muhtasari

•Kanisa hilo limekuwa makao kwa “wagonjwa” wenye matatizo ya akili ambao wamepelekwa kanisani na wapendwa wao kupata “uponyaji” lakini wanazuiliwa kinyume na matakwa yao.

•Upande wa kanisa ulisema, "“Tunawapa magodoro lakini wengi wao huishia kuyachana, kula au kujinyima. Kuna kidogo tunaweza kufanya kuhusu hilo,”

Image: BBC

Kanisa moja Katoliki kwenye barabara kuu ya Kisumu-Kakamega nchini Kenya, limegunduliwa kuwa na wagonjwa wanaozuiliwa humo kwa ajili ya kupata maombi.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na chombo cha habari cha NTV, kanisa hilo limekuwa makao kwa “wagonjwa” wenye matatizo ya akili ambao wamepelekwa kanisani na wapendwa wao kupata “uponyaji” lakini wanazuiliwa kinyume na matakwa yao.

NTV imebaini kuwa watu wasio na hatia wamekuwa wakifungwa minyororo na kunyimwa chakula kama inavyostahili, huku wakiwa wanaishi kwenye maeneo yaliyotengwa.

Wakati wanaingia kwenye kanisa hilo wakiwa wameandamana na maafisa wa polisi, baadhi ya matukio waliokutana nayo ni pamoja na kukutana na waathiriwa “wagonjwa” wakiwa kwenye mazingira mabaya, kama vile wanapolala hakuna hata magodoro, wanajisaidia kwenye ndoo na kadhalika, kulingana na NTV.

Hata hivyo kulingana na NTV, upande wa kanisa ulisema,

“Tunawapa magodoro lakini wengi wao huishia kuyachana, kula au kujinyima. Kuna kidogo tunaweza kufanya kuhusu hilo,” alisema kasisi Jared.

Insemekana kuwa sababu za wanaoletwa hutofautiana ikiwemo walioathirika na mihadarati.

Aidha, kiongozi wa kanisa hilo la Coptic Holy Ghost Church Father John Pesa, alizungumza na vyombo vya habari na kusema:

“Hatujawateka nyara watu hawa na kuwaleta hapa. Ni familia zao zinazowaleta kanisani. Hakuna ubaya kuombea watu wapone.”