Alimuua mumewe kimakosa, akahukumiwa kunyongwa, akanusurika jela miaka 24 baadae!

Akihukumiwa kunyongwa, alikuwa mjamzito wa mtoto wa 5 na pia alikuwa anaugua saratani. Alijifungua akiwa jela na mtoto wake alifariki miaka kadhaa baadae ila hakuruhusiwa kwenda kumzika.

Muhtasari

• Rukilwa alisema kuwa hakudhamiria kumuua mume wake, kwani wakikuwa wanang'ang'ania shoka na mumewe akajikata kichwa kwa shoka hilo.

• Hata baada ya kutoka jela baada ya miaka 24, watoto wake wote walimkataa wakiaminishwa kuwa alimuua baba yao kwa kupenda.

Robinah Rukilwa, mama ambaye alikiri kumuua mumewe, akahukumiwa kunyongwa, akanusurika jela baada ya miaka 24 lakini nyumbani watoto wake wakamtoroka.
Robinah Rukilwa, mama ambaye alikiri kumuua mumewe, akahukumiwa kunyongwa, akanusurika jela baada ya miaka 24 lakini nyumbani watoto wake wakamtoroka.
Image: screengrab

Robinah Rukilwa, mama ambaye alihukumiwa kifo lakini baadae akakwepa hukumu hiyo na kuhudumia kifungo cha miaka 24 jela badala yake kwa kosa la kumuua mume wake, amefunguka upande wake wa hadithi, miaka mitatu baada ya kutoka jela.

Mama huyo ambaye alizungumza kwenye mahojiano ya kuliza na chaneli moja ya YouTube alisema kuwa baada ya kwenda jela, watoto wake walimchukia hata baada ya kumaliza kifungo cha miaka 24 hakuna anayetaka kumkaribia, kwa kile alisema kuwa ndugu wa mume wake waliwashawishi kuamini kwamba ni yeye alimuua baba yao, ambaye ni mume wake.

Ilikuwaje mpaka kujipata jela?

Rukilwa alisema kuwa ni kweli kifo cha mume wake alikisababisha yeye, lakini si kwa kudhamiria.

Kulingana naye, mume wake alikuwa msumbufu sana na mlevi ambaye alikuwa anauza mali yao na kwenda kulewa nayo, na anaporudi nyumbani alikuwa ni mkorofi kupindukia.

“Wakati niliolewa, nilidhani mume wangu ni mtakatifu, alikuwa na tabia nzuri, lakini miaka michache baadae, alianza kuwa mkorofi. Alikuwa ananipiga mpaka nabubujikwa na damu, na mpaka leo hii niko na baadhi ya majeraha hayo,” Rukilwa alisema akionesha majeraha hayo huku machoni machozi hayaachi kumtiririka.

Alisema kuwa kipigo na manyanyaso haya yalidumu kwa miaka 10 akiwa mvumilivu hadi pale mzee wake alizidi na kuanza kuuza mali ikiwemo mifugo na hata shamba, na hela zote kuzipeleka ulevini.

Alipojaribu kumkanya, mumewe aligeuka mbogo na kumpiga vibaya kiasi kwamba alijinyasua mikononi mwake na kukimbilia kwao akiwa na watoto wanne.

Lakini nyumbani kwao hakutakiwa kule na wazazi wake walimkaripia wakimtaka arudi kwa mumewe. Rukilwa hakuwa na jinsi.

Aliamua kurudi na watoto wake wanne, na kipindi hicho alikuwa na ujauzito wa mtoto wa tano. Aliwarudisha angalau kuwa na baba yao.

Usiku mmoja mumewe mlevi chakari alifika nyumbani kwa shari zote akiwa na shoka mkononi ambalo kulingana na Rukilwa alikuwa amenuia kulitumia kumuangamiza yeye.

Alipoingia kwa nyumba, alianza kumtafuta gizani mke wake, akiwa na lengo la kumpasua kichwa na Rukalwa alijisatiti kujaribu kujinasua na kumpokonya shoka lile.

Kulingana naye, anashuku kipindi hiki ndipo mumewe alijikata na shoka kichwani, katika hali ya kung’ang’ana na yeye alijinasua na kukimbilia maisha yake bila kujua kwamba mumewe alikuwa ameanguka chini kutokana na kulemewa kwa majeraha ya shoka lile.

“Nilifanikiwa kujinasua na kutoroka na alinifuata mbio lakini hakuweza kunifikia. Baadae asubuhi watu walikuja nyumbani wakiniuliza nini kilimtokea. Waliniambia waliona mwili wake ukiwa sakafuni bila dalili ya uhai. Na hivyo ndivyo nilijua kwamba amekufa,” Rukilwa alisema kwa uchungu.

Wanakijiji walitaka kumuua lakini ndugu wa mumewe mdogo aliingilia kati na kuita chombo cha dola, na hivyo ndivyo safari yake ya gerezani.

Ifahamike kwamba kipindi anapelekwa kituo cha polisi kusubiria mashtaka ya mauaji ya mumewe, Rukilwa alikuwa na ujauzito wa mtoto wa 5, na alikuwa pia anaugua saratani ambayo ilikuwa imefikia daraja la 4.

“Nilihukumiwa kunyongwa katika mahakama ya juu, nikaenda katika mahakama ya rufaa wakaniambia niende nife, nikakata rufaa tena katika mahakama ya upeo wa juu ambapo pia walidumisha hukumu huo huo wa kunyongwa,” alisema.

Akiwa jela, Rukilwa alijifungua mtoto wake wa tano ambaye alilazimika kumlea katika mazingira mabaya ya gerezani bila nguo, chakula kizuri na malazi salama kwa mtoto hadi pale alipoacha kunyonya na akachukuliwa kwenda kulelewa katika kituo cha kulea watoto wasio na wazazi.

Kipindi hiki chote, alikuwa anasoma Biblia kila wakati, akisubiria kunyongwa kama ambapo mahakama za ngazi zote zilivyoamua.

Wakati huo huo pia saratani ilikuwa imemlemea lakini alitibiwa.

Kipindi hicho pia ndio yule mtoto wake alifariki bila kupewa taarifa wala kupewa nafasi ya kwenda kumzika mwanawe aliyemzaa gerezani, Rukilwa alikumbuka hili kwa machozi mengi.

Alikuwa amehudumia kifungo cha miaka 16 jela na hapo ndipo hakimu alijitolea kurejelea kesi yake na aligunduliwa kuwa hakuhusika moja kwa moja katika kesi ya mauaji ya mumewe bali ilikuwa ni ajali wakati wa makabiliano.

Jaji alimpunguzia adhabu yake kutoka kunyongwa hadi kuhudumia miaka 24 jela – lakini tayari alikuwa amekaa jela miak 16, kwa hiyo alikuwa na miaka 8 zaidi ili kumalizia kifungo chake na kuwa mtu huru.

Baada ya miaka 8 kukamilika, Rukilwa alikuwa mtu huru, lakini nje ya jela hakuna mtu aliyetaka kuwa karibu naye, kila mtu akiwa ameamini kwamba alikuwa muuaji.

Kulingana na simulizi yake, watoto wake 4 ambao aliwapata sasa ni watu wazima, walimtelekeza na kutotaka kumuona wakiamini kuwa ndiye aliua baba yao.

Rukilwa alikuwa na maneno haya kwa wanawe;

“Wanangu, nawaombea Mungu awabariki, awawezeshe kwa kila kitu. Mlinichukia na kulaumu damu ya baba yenu kwangu, lakini katika ukweli, hivyo ndivyo Mungu alikuwa amepanga kifo chake. Sikudhamiria kumuua,” alisema kwa huzuni na moyo mzito wenye hisia za majonzi.

Rukilwa sasa anasema anaishi peke yake pasi na mtu yeyote kutaka hata kumpa kibarua ili kujipatia chakula na mahitaji ya kila siku, huku akisema kuwa vibarua vya kufulia watu nguo ndivyo amekuwa akifanya lakini anaumia mgongo kwani umri pia umekwenda.

Mama huyo anaomba msaada wa kifedha kuweza kujikimu na pia yeyote ambaye anaweza kumpatanisha na wanawe.