Simulizi: Nilifungwa jela miezi 12 kwa kuiba sigara, ndio bado mwezi ila jela si kuzuri!

"Ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kuiba...” Macharia ambaye alikuwa amekaa jela kwa mwezi mmoja alisimulia kwa majuto makuu.

Muhtasari

• Kando na pakiti ya sigara, Macharia pia alichomoa kiboksi kidogo kilichokuwa na kadi za vocha ya mjazo wa simu.

Mfungwa akiwa jela
Mfungwa akiwa jela
Image: Mfungwa Jela

Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 25, Samwel Macharia kutoka Githunguri amesimulia hadithi yake ya kusikitisha jinsi alijipata kutumikia kifungo gerezani kwa kosa la kuiba sigara.

Macharia ambaye alikuwa anasimulia kutoka gereza la wanaume la Kiambu alisema kuwa kwao ni Githunguri na alifanya udhubutu wa kuiba sigara katika jaribio lake la kwanza kwenye wizi na kosa hilo likamtupa jela.

Kulingana naye, alifika katika duka la muuzaji mmoja na akamvizia waakti alikuwa anauzia wateja wengine, akaingiza mkono na kuchomoa pakiti ya sigara na kwenda nayo.

Kando na pakiti ya sigara, Macharia pia alichomoa kiboksi kidogo kilichokuwa na kadi za vocha ya mjazo wa simu.

“Mimi nilishikwa nikiwa kwa baze ya bangi, nilibia mtu sigara… alikuwa anauza kwa duka sasa nikam time kama ameweka pikipiki kando yake, akiendelea kuuzia mtu, nikachukua hiyo pakiti pamoja na vocha ya mjazo wa simu nikaenda nazo…. Ndio ilikuwa mara ya kwanza…..” Macharia ambaye alikuwa amekaa jela kwa mwezi mmoja alisimulia.

Aliondoka nazo na mwenye duka wala hakumfuata kumuuliza, siku moja baadae ndio alikujiwa na polisi na wakamtia ndani ya gari la kumpeleka katika kituo cha polisi cha Githunguri na kutoka hapo akapelekwa mahakamani na kuhukumiwa kifungu cha mwaka mmoja.

Macharia alisema kuwa awali alikuwa amepewa adhabu ya kifungo cha nje, baada ya kumzengua mama yake nyumbani kwa kumwaga maziwa, lakini hakuzingatia kifungo hicho na alipopatikana na kosa la pili, alipewa adhabu ya jumla ambayo ilikuwa mwaka mmoja.

Macharia alisema nyumbani walikuwa wanashirikiana na mama yake katika ukulima wa ng’ombe wa maziwa na kuku wa mayai.

“Nilikuwa nimeshtakiwa na mama kwa kumwaga maziwa, nikachanganyishiwa ndio ikakuja mwaka mmoja….” Alisema.

Kijana huyo aidha alikiri kwamba amekuwa ni mtoto mtukutu kwa mama yake alisema baada ya kifungo cha mwezi jela, amebadilika na iwapo ataonewa msamaha afunguliwe baada ya kuhudumu miezi sita, atakuwa mtu mzuri na wa maana nyumbani na katu hatoweza kujihusisha na utundu wala wizi tena.

“Nimekuwa ni mtu wa kusumbua sana lakini sasa nitarekebika kwa vile sijawahi kuja hapa, nitakuwa nimejifunza,” Macharia alisema.