Moses Kuria motoni baada ya kutusi chombo cha habari vibaya, kuomba idara za serikali kukisusia

Matamshi ya Kuria ya Jumapili yamezua ghadhabu nyingi kutoka kwa wanamitandao Wakenya.

Muhtasari

•Kuria alizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumapili baada ya kudaiwa kuchapisha ujumbe wa matusi dhidi ya jumba moja la habari maarufu nchini.

•Kuria alidai kuwa shirika hilo la habari limechukua majukumu ya upinzani na kulitaka lieleze ikiwa bado ni shirika la habari.

WAZIRI MOSES KURIA
Image: TWITTER

Waziri wa Biashara, Moses Kuria amejipata pabaya kufuatia chapisho la kutatanisha kwenye akaunti yake ya Twitter siku ya Jumapili jioni.

Mbunge huyo wa zamani wa eneo la Gatundu alizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumapili baada ya kudaiwa kuchapisha ujumbe wa matusi dhidi ya jumba moja la habari maarufu nchini.

“…. Bado mnaweza kutangaza dalali na matangazo ya mazishi. Hatutazuia hizo,” waziri huyo alisema kwenye Twitter.

Kauli hiyo ilikuja saa chache tu baada ya waziri huyo kuziagiza idara zote ya serikali kususia Nation Media Group.

Wakati akitoa hotuba katika hafla moja katika kaunti ya Embu, mwaniaji huyo wa zamani wa ugavana alidai kuwa shirika hilo la habari limechukua majukumu ya upinzani na kulitaka lieleze ikiwa bado ni shirika la habari.

"Nation Media, muamue kama nyinyi bado ni gazeti ama shirika la habari ama ni chama cha upinzani. Na mimi nimesema, kutoka kesho, kutoka leo sio kesho, idara yote ya serikali nitaona imeweka tangazo kwenye Nation Media, ujihesabu uko nyumbani. Mungu awabariki na awatendee mema," waziri alisema.

Matamshi ya waziri Moses Kuria ya siku ya Jumapili yamezua ghadhabu nyingi kutoka kwa wanamitandao Wakenya.

Wakenya wameendelea kumkosoa huku wengi wakishangaa kwa nini afisa mkuu wa serikali alitumia maneno makali namna hiyo hadharani.

@cbs_ke Waah! je huyu ni Mheshimiwa Moses Kuria ametweet? Natilia shaka?

@mason_knows Waziri wenu wa Biashara. Ni hawa mnategemea

@Asamoh_ Dalili ya Hatia na ufisadi. Tunasimama na vyombo vya habari. Ukweli unaowasilishwa na waandishi wa habari unaweza tu kupingwa kwa ushahidi na sio matusi mabaya.

@abuga_makori Dkt Ruto anafaa kuwapa adabu mawaziri kama hawa wanaofanya utawala wake uonekane wa kidikteta. Moses Kuria amelegea mdomoni. Vyombo vya habari vya Nation vinaweza kuwa vilipotosha ukweli lakini uungwana ni muhimu sana.

Hata hivyo, baadhi ya wanamitandao walionekana kumtetea waziri huyo huku baadhi wakidai shirika hilo la habari lilikosea.