Kwa nini vipimo vya uzazi vinazua hofu nchini Uganda

Tajiri huyo na familia yake hawajawahi kuzungumzia hadharani suala hilo, na ripoti hiyo haijathibitishwa.

Muhtasari
  • Kliniki za kibinafsi pia zilipokea pesa kwa mtindo huo, zikiweka matangazo kwenye mabango kunadi huduma hiyo.

Ripoti za ongezeko kubwa la wanaume wanaotafuta vipimo vya uzazi, zimeibua hofu kuwa huenda ikasambaratisha familia na kuwaacha watoto na madhara ya kisaikolojia.

Suala hilo limezu gumzo nchini humo tangu gazeti moja lilipochapisha taarifa inayodai kuwa mfanyabiashara mmoja maarufu - ambaye alikuwa na wake kadhaa - aligombana na mmoja wao, na kumfanya atafute vipimo vya uzazi ambavyo vinadaiwa kuthibitisha yeye ni baba wa watoto wake 15 kati ya 25.

Tajiri huyo na familia yake hawajawahi kuzungumzia hadharani suala hilo, na ripoti hiyo haijathibitishwa.

Lakini taarifa hiyo ilienea kama moto wa nyika na imezua mzozo mkubwa katika miezi michache iliyopita, na kusababisha baadhi ya wabunge kutoa wito kwa wanaume kuacha kuweka familia katika katika hali itakayowaathiri kisaikolojia.

"Hebu tuishi kama walivyoishi mababu zetu. Mtoto aliyezaliwa nyumbani ni mtoto wako," Waziri wa Maendeleo ya Madini Sarah Opendi alisema bungeni.

Ingawa alithibitisha kauli yake kwa kuongeza kwamba ikiwa mwanamume alitaka vipimo vya uzazi unapaswa kufanywa wakati mtoto anazaliwa - sio akiwa mtu mzima.

Cha kusikitisha zaidi ni kwamba, gazeti la kibinafsi la Monitor liliripoti kuwa upimaji huo umesababisha vurugu za kinyumbani, ambapo polisi wanamkamata raia wa Israel anayeishi nchini Uganda kwa madai ya kumuua mkewe baada ya matokeo ya DNA kuonyesha kuwa yeye si baba wa mtoto wao wa miezi sita. Mwanaume huyo bado hajafunguliwa mashtaka.

Akizungumza katikati ya mwezi Julai, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Simon Mundeyi, alisema kumekuwa na ongezeko la mara 10 la maombi ya vipimo, ambayo yanahitaji kuchukuliwa DNA ya baba na mtoto.

"Tulikuwa tukipokea maombi 10 kila siku katika maabara yetu ya uchambuzi ya serikali. Sasa tuna karibu 100 kila siku na idadi bado inaongezeka," aliongeza.

Kliniki za kibinafsi pia zilipokea pesa kwa mtindo huo, zikiweka matangazo kwenye mabango kunadi huduma hiyo.

Hili lilizua wasiwasi kwamba huenda matokeo yakageuka kuwa sio sawa, haswa baada ya ripoti kuibuka kuwa vifaa vya kupimia vilivyoshukiwa kuwa ghushi viliingizwa nchini Uganda.

Wizara ya Afya iliingilia kati ili kudhibiti upija wa kiholela wa uzazi na kutoa idhini kwa maabara tatu tu zinazoendeshwa na serikali - ingawa mkurugenzi wa afya ya umma, Daniel Kyabayinze, alisema gumzo kubwa la kuongezeka kwa idadi ya watu wanatafuta huduma hiyo lilikuwa mitandaoni.

Hata hivyo, hatua zilikuwa zikichukuliwa ili kuhakikisha kuwa familia zinapata ushauri nasaha na usaidizi wa kisaikolojia wakati vipimo vilipofanywa.

"Tumeona ujumbe mitandaoni ambapo watu wanahisi vipimo vya uzazi vinatatiza familia na vinaweza kusababisha unyanyasaji wa kijinsia. Tunataka kuhakikisha hilo halifanyiki kwa sababu ya matokeo ya vipimo hivuo," Dkt Kyabayinze aliambia BBC.

Mjadala huo ambao umepamba moto kote nchini Uganda umepokelewa kwa hisia mseto - kuanzia kenye mabaa hadi Bungeni; kwenye magari ya uchukuzi wa umma hadi mtanzao wa Twitter, ambayo sasa inajulikana kama X.

Akielezea kuunga mkono vipimo hivyo, mkazi wa Kampala Bwette Brian aliambia BBC: "Nadhani mwanamume huyo ana haki ya kujua kama watoto ni wake au la. Watoto ni wajibu na kila mtoto lazima ajue familia anayoshikamana nayo."

Akitofautiana, mkazi mwingine, Tracy Nakubulwa, alisema: "Nimeona ndoa zenye furaha na familia zikisambaratika kutokana na suala la kupima uzazi - na watoto wanakuwa waathirika."

Mwanaharakati wa haki za binadamu Lindsey Kukunda alisema ukweli kwamba wake wakati mwingine wana uhusiano wa siri na mwanamume mwingine, kumbambikizia mumewe mtoto, "sio jambo jipya".

"Babu zetu walifanya hivyo, mama zetu walifanya hivyo," alisema.

Anabainisha kuwa wanandoa wanapopata shida ya kupata watoto, mara nyingi mwanaume ndiye anakuwa na matatizo ya uzazi, ambapo “katika tamaduni za Kiafrika, mwanamke asipokuw ana uwezo wa kupata watoto, ataachwa au atafukuzwa nyumbani” .

"Kwa hiyo kile ambacho wanaume hawa hawatambui ni kwamba wanawake waliowazalia watoto wamelala na wanamume mwingine - ili wawapatie mtoto wanaowatamani."

Bi Kukunda aliwashutumu wanaume wanaofanya vipimo vya uzazi kwa kuzingatia hoja mbili.

"Ni kawaida kwa wanaume kuwa na mahusiano na kuleta watoto nyumbani - lakini wake wanalea watoto hawa kama wao," alisema.