Kawira Mwangaza ni nani? Mfahamu kwa undani Gavana wa Meru aliyeponea kubanduliwa mara mbili

Kawira amenusurika kubanduliwa mara mbii, Desemba 2022 na Novemba 2023.

Muhtasari

•Jumatano jioni, Bunge la Seneti lilitupilia mbali ombi la kumtimua gavana wa Kaunti ya Meru, Kawira Mwangaza.

•Kawira ana Digrii ya Elimu katika Uongozi na Ushauri kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, nchini Uganda.

GAVANA WA MERU KAWIRA MWANGAZA
Image: EZEKIEL AMING'A

Siku ya Jumatano jioni, Bunge la Seneti lilitupilia mbali ombi la kumtimua gavana wa Kaunti ya Meru, Kawira Mwangaza.

Maseneta walipiga kura ya kutupilia mbali mashtaka yote saba yaliyoibuliwa dhidi ya gavana huyo na Bunge la Kaunti ya Meru baada ya kusikilizwa kwa siku mbili.

Gavana huyo wa muhula wa kwanza alitimuliwa madarakani baada ya MCAs 59 kupiga kura ya kuunga mkono hoja ya kumuondoa madarakani mwezi uliopita.

Siku ya Jumatano, seneti ilijadili kuhusu ushahidi uliotolewa na timu ya wanasheria wa Bunge la Kaunti ya Meru na utetezi wa Mwangaza miongoni mwa masuala mengine. Mapema Jumanne, gavana alikuwa amekanusha mashtaka yote saba ambayo yaliletwa dhidi yake na MCAs wa kaunti.

Hii ni mara ya la pili ambapo Kawira amenusurika kung'olewa madarakani baada ya la kwanza kutupiliwa mbali na Bunge la Seneti mwishoni mwa mwaka jana.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo huenda hujui kuhusu gavana huyo mwanamke shupavu wa Kaunti ya Meru ambaye amenusurika kubanduliwa mara mbili katika kipindi cha mwaka mmoja.

  • Alizaliwa mwaka wa 1973.
  • Alifunga ndoa na mwanamuziki Murega Baichu, Mei 2018.
  • Ni askofu katika Kanisa la Baite Family Fellowship.
  • Anamiliki kituo cha  Baite TV na Baite FM pamoja na mumewe.
  • Alikuwa kijakazi baada ya Shule ya Msingi.
  • Ana Digrii ya Elimu katika Uongozi na Ushauri kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, nchini Uganda.
  • Aliwania ubunge wa eneo la Buuri mwaka wa 2013 ila akashindwa.
  • Alikuwa Mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Meru (2017-2022)•
  • Alichaguliwa gavana wa Kaunti ya Meru, Agosti 2022.
  • Amenusurika kubanduliwa mara mbii, Desemba 2022 na Novemba 2023.