Kasisi anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja: 'Nililia nilipolipata kanisa hili'

Kanisa moja nchini Kenya limekuwa likiendesha shughuli zake kisiri kwa muongo mmoja uliopita.

Muhtasari

• Halitangazi huduma zake kihafidhina kwa sababu inawapokea washirika ambao ni wapenzi wa jinsia moja.

Kanisa moja nchini Kenya limekuwa likiendesha shughuli zake kisiri kwa muongo mmoja uliopita. Halitangazi huduma zake katika nchi hiyo ya kihafidhina kwa sababu inawapokea washirika ambao ni wapenzi wa jinsia moja.

"Mara ya kwanza nilipoingia kanisani nililia," John, mchungaji aliyetawazwa awali katika kanisa kuu, aliambia BBC.

Aliiacha parokia yake kwa sababu viongozi wa kanisa walimwambia jinsia yake ni dhambi na kwamba alihitaji kusalia mseja.

"Sikuwahi kufikiria maishani mwangu kama kasisi, ningekuwa katika nafasi ambayo ningesema maneno matatu ambayo watu wanadhani yanakinzana. Kwamba mimi ni mwafrika, mimi ni mpenzi wa jinsia moja, mimi ni padri."

Alipata habari kuhusu kanisa hilo la kisiri, ambako sasa anahubiri, kwenye mitandao ya kijamii - ingawa wengi wanapata neno moja kwa moja kanisani. Kama wote waliohojiwa kanisani, jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake.

Washirika wake pia wanalindwa sana kuhusu kushiriki maelezo ya mikusanyiko yao - wale wanaotaka kujiunga wanakaguliwa kwa uangalifu kabla ya kualikwa ili kuhakikisha kuwa sio mtego au mtu mbaya.

Maelewano na waumini wote ni kwamba ulinzi na usalama ni muhimu.

Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Kenya, ambako jamii nyingi ni za kihafidhina. Mwaka huu Mahakama ya Juu ilibatilisha marufuku dhidi ya wanachama wa jumuiya hiyo kujiandikisha kama mashirika yasiyo ya kiserikali.

Hata hivyo kanisa hili halitashawishika kujiandikisha kutokana na kuongezeka kwa hisia kali dhidi ya LGBT - ukizingatia pendekezo la hivi majuzi la mbunge mmoja la kuimarisha sheria dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.

Makanisa yanayotoa huduma inayokumbwa na utata huwa yanajitambulisha kuwa yale ambayo yanajitolea hadharani na kujumuisha watu wa mielekeo yote ya kijinsia kijinsia kimakusudi, hasa wale walio katika jumuiya ya LGBTQ, bila chuki yoyote. Pia wanafanya kazi ya kuwatafutia haki.

Ninapojiunga na ibada siku ya Jumapili yenye utulivu, muziki taratibu unasikika kutoka kwenye chumba cha jengo lisilo la kawaida.

Watu huanza kuingia ndani hadi wanafika 30 au zaidi.

"Tunakaribia kuanza. Naomba, tufunge macho yetu na kutafakari," anasema Pauline, mhudumu aliyevalia vazi refu jeusi na kitambaa chekundu. Chumba kizima kimya.

Pauline ni mpenzi ya jinsia moja, ambaye anatumia neno "wao" kama kiwakilishi chaa kibinafsi, na ni mmoja wa waanzilishi wa kanisa. Hapo awali ilikuwa ni marafiki wachache tu walikusanyika ili kusaidiana.

"Unapoondolewa kwenye nafasi [kanisa], kuna hamu ya kujua kama kuna mtu mwingine yeyote ambaye ametengwa," anasema Pauline, ambaye hakutengwa lakini hakuhisi kuwa anakubalika katika makanisa makuu.

"Tulitaka kujumuika na Wakristo wengine wa ajabu ambao wanajithibitisha wenyewe."

Wale wanaohudhuria kanisa hilo wamejifunza kuwa inawezekana kujivunia kuwa Mwafrika, Mkristo na kuwa mpenzi wa moja
Wale wanaohudhuria kanisa hilo wamejifunza kuwa inawezekana kujivunia kuwa Mwafrika, Mkristo na kuwa mpenzi wa moja

Hisia ya kutengwa ilikuwa imetawala maisha ya Pauline, hasa tangu baba yao alipofariki kutokana na VVU/Ukimwi walipokuwa na umri wa miaka 12.

"Baada ya baba yangu kufariki watu walianza kututenga, walidhani sisi sote tuna Virusi Vya Ukimwi. Mama yangu angehudumiwa kwa vikombe na sahani tofauti na tulizuiwa kuingia katika sehemufulani. Kanisa ni moja ya sehemu ambazo hatukuweza kuhuduria kwa sababu watu waliamini mama yangu alikuwa 'mchafu'," Pauline anasema.

Kutengwa huko kukawa mtindo maisha, huku kila kanisa likionekana kuhoji kipengele fulani cha maisha ya Pauline - iwe ni jinsi alivyovaa au kwa nini alichagua kutokuwa katika uhusiano wa kawaida.

Kwa hivyo Pauline na marafiki zake walianza kukutana Jumapili ili kutazama mahubiri kwenye YouTube huku wakiwafikia Wakenya wengine wa LGBT pia.

Ni wakati huo ambapo hisao kali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ilikuwa ikiongezeka Afrika Mashariki. Nchi jirani ya Uganda ilikuwa inaanza mjadala wa kuwasilisha sheria mpya ya kupinga mapenzi ya jinsia moja - ambayo imeimarishwa zaidi.

Kile ambacho hawakufikiria ni kwamba miaka 10 baadaye mkusanyiko wao mdogo ingekua na kujumuisha zaidi ya washirika 200.

Wengi wao wamepata msukumu wa kuondoka katika sehemu zao za ibada za awali.

Kwa Regina, ilifuatia makabiliano makubwa na mfanyakazi mwenzake wa kujitolea - sehemu ya kundi lililopanga matukio katika kanisa lake.

Jumuiya hiyo ya vijana wa kanisa ilimpa makataa ya kuondoka ilipogundua kuwa alikuwa na rafiki wa kike: yeye au wao.

"Nilihisi kama nimesalitiwa. Kwani nilikuwa nimewashauri baadhi yao na sasa, sikuweza kuwa sehemu yao tena. Hapa kulikuwa na watu ambao hawakuweza kueneza neema kwa watu walio tofauti," anasema.

Regina alichagua kusalia na mpenzi wake. Muongo mmoja baadaye, akitamani kuunganishwa tena na imani yake ya Kikristo na jumuiya, safari yake ilimpeleka kwenye kanisa la uthibitisho wa hali ya juu.

"Kuna wakati nilihisi kama sina njia ya kumkaribia Mungu. Nilichowahi kusikia ni kwamba mimi ni mwenye dhambi. Ikiwa maombi ni njia ya kuzungumza na Mungu, ningewezaje kuomba? Kurudi katika jumuiya ya watu wenye imani kumenisaidia kutuliza maumivu ya zamani," anasema.

Baada ya miaka 10 kanisa hilo sasa lina zaidi ya washirika 200
Baada ya miaka 10 kanisa hilo sasa lina zaidi ya washirika 200

Hata hivyo si rahisi kila wakati kwa mkusanyiko, ambao umekabiliwa na mashambulizi kadha wa kadha- kwa mfano wakati mwenye nyumba au wale walio katika jumii inayowazunguka wakigundua kwamba wanakubali washirika wa LGBT.

Wamefungiwa nje ya majengo licha ya kulipa kodi, boma lao limeibiwa, wanachama kushambuliwa na polisi wameomba rushwa ili kuwapa "ulinzi" au kutishia kuwapiga na kuwakamata.

Wamebadilisha maeneo mara tisa katika miaka yao 10 ya uwepo wao, ili kuweka siri eneo lao la ibada.

Licha ya changamoto hizo kanisa hilo limekuwa likiwasaidia washirika kuungana tena na imani yao na jamii ambayo wanahisi imejaribu kuwatenga.

Kanisa, kwa mfano, lina toleo lake la Imani ya Mitume, ambayo inakaririwa na washirka wakati wa ibada, kwa kawaida huanza na maneno: "Ninaamini katika Mungu, Baba Mwenyezi, Muumba wa mbingu na dunia." Inaendelea kwa undani kueleza msingi wa imani yao.

"Sote tulipenda imani ya kawaida, lakini kulikuwa na mambo ambayo yalikosekana," anasema Pauline.

"Wanawake hawatambuliki na kama watoto wa kitambo, tulilazimika pia kujiweka katika imani. Tunamwona Mungu baba na mama. Inathibitisha kila mtu."

Mstari wa kwanza wa imani yao unasema: "Tunaamini katika Mungu mmoja, Muumba wetu, chanzo cha kuwa kwetu kama watoto wapendwa."

Kanisa limerekebisha Imani ya Mitume
Kanisa limerekebisha Imani ya Mitume

Ratiba ya kanisa pia inaweza kubadilika kwani baadhi ya waumini hawajafahamisha familia na marafiki kuhusu muelekeo wao wa kijinsia, kwa hivyo wanahudhuria makanisa ya kawaida kabla ya kujiunga na ibada yake baadaye.

"Tulipoanza, kila mtu alikuwa na hofu na hakuna aliyekuwa tayari kuelezea kile anachopitia maishani," Pauline anasema.

Hii ilihamasisha "Chat and Chew", kongamano la majadiliano ambalo huruhusu washirika kuangazia maisha yao bila hofu kwa Wakenya wenzao katika jumuiya ya LGBT.

“Baada ya ibada, watu wengi walikuwa wakiwatafuta wachungaji ili wasimulie madhila wanayopiti kutokana na mahusiano yao, kutengwa na familia, kukosa makazi na changamoto nyingine nyingi ambazo watu wenye muelekeo huu wa kijinsia wanapitia, na kutiana moyo na kuponya."

Lakini huku mazingira nchini Kenya yakizidi kuwa ya chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja , Pauline anasema baadhi ya washiriki wamefikiria kujificha kwa usalama wao - ingawa wengi wanataka kanisa liendelee.

"Tulipoanza, hatukufikiria kuwa sehemu hii ingekuwa muhimu sana. Lakini hatuwezi kukata tamaa, lazima tufikirie njia ya kusonga mbele.

"Nataka sehemu hii iwe wazi kwa kila mtu na kupata usawa ambapo sote tunaheshimiana licha ya imani na mila zetu."

Majina yote yamebadilishwa ili kulinda utambulisho.