Mauti na udanganyifu, Suala la Shakahola na itikadi kali za Kidini

Baadhi ya wachungaji wanatumia dini kujistawisha

Muhtasari

•'’Mimi nashangaa vile serikali imeamua kutuficha katika suala hili sugu linalohusisha maisha na uhai.''

•''Mimi siendi church kwa sababu ninapotoa sadaka namfaidi mchungaji wala sio jamii.''

• Ingawa muda umepita,kwa wengine jinamizi la Shakahola linakaa la jana.

Miili ya walioaga Shakahola
Image: MAKTABA

Mwaka jana taifa la Kenya lilipigwa na butwaa baada ya miili zaidi ya 600 kufukuliwa katika eneo la Shakahola, kiini cha vifo vyao ilikuwa imani potovu.

Inasemekana kuwa, waumini hawa walikuwa wanafuata dini ya mchungaji mmoja kwa jina Mackenzie ambaye alikuwa amewaeleza kuwa wakitaka kumuona Mwenyezi Mungu wafunge kwa muda wa siku arobaini jinsi Kristo alivyofanya kwenye maandiko matakatifu ya Biblia.

Naam, baadhi ya waumini walianza kufunga na wengi wao walipoteza Maisha kutokana na ukosefu wa maji wa chakula kwenye miili yao.

Mwaka mmoja baadaye,licha ya serikali kutoa maagizo ya namna dini itakavyoendeshwa, bado wachungaji wanazidi kutumia dini kuendeleza propaganda zao za maovu na utapeli.

''Mimi siendi church kwa sababu ninapotoa sadaka namfaidi mchungaji wala sio jamii,'' ndiyo iliyokuwa kauli ya bwana Emmanuel Shivachi.

Suala la Shakahola bado ni donda ndugu kwa jamaa na familia ya waliopeteza wapendwa wao. 

Yakini, wengi wamenyamaza na kutupilia mbali suala hili la uhayawani na upotoshaji wa waumini ila kwa wengine bado tukio hilo ni donda sugu kwenye mitima yao na ingawa muda umepita,kwa wengine jinamizi la Shakahola linakaa la jana.

‘’Mimi nashangaa vile serikali imeamua kutuficha katika suala hili sugu linalohusisha maisha na uhai.Hata baada ya Mackenzie kupotosha waumini bado haki kamili haijatimia!'' Familia moja ilisema kwa simanzi.

Licha ya serikali kuwekeza vidhibiti katika ufunguzi wa makanisa, baadhi ya waja wanazidi kuwapotosha waumini wakitumia dini ili kujinufaisha wao binafsi.

Kwa mfano, mchungaji mmoja kwa jina Wafula anayetoka katika kaunti ya Kakamega, alijishindia milioni mia moja katika mchezo wa Kamari ambapo alifungua mangweni na kuacha shughuli zake za kuhubiri.

Hili liliwawacha wengi vinywa wazi hasa washiriki wa kanisa lake. Vilevile aliwaambia waumini hao wajitafutie riziki namna alivyofanya.

Ni mtindo ambao umegeuka kuwa wa mazoea hasa katika karne ya ishirini na moja ambapo insi wengi wanatumia dini kuendeleza matakwa yao ya ubinafsi.

Katika kukuru kakara na patashika za ulimwengu, hali hii imechochea kua kwa waumini mbalimbali wanaoamini maneno yanayotoka kwenye vinywa vya wachungaji wao ambao wengine ni walaghai, waongo na wadanganyifu.

Katika biblia na kurani takatifu mwenyezi Mungu ndiye chanzo cha maisha na hasa ndiye aliye na uwezo wa kuweka na kutoa.

Hata hivyo inasikitisha kuwa wachungaji wengi wanatumia maandiko na wamegeuza dini takatifu kwa manufaa yao binafsi.

Jambo la dharura lisipofanywa basi huenda tukawapoteza wengi kutokana na huu upotoshaji na ulaghai.