Kwa nini Ruto hakuwa na chaguo bali kulivunja baraza la mawaziri?

Ruto anasema alichukua uamuzi huo baada ya kuwasikiliza wananchi na kwamba ataunda serikali pana baada ya mashauriano.

Muhtasari
  • Haya yanajiri licha ya madai ya serikali kwamba ilipata hazina ya serikali ikiwa tupu ilipochukua madaraka.
RAIS WILLIAM RUTO
Image: PCS

Rais  William Ruto siku ya Alhamisi alivunja baraza lake la mawaziri na kuwafuta kazi mawaziri wake wote huku akiahidi kuunda serikali mpya ambayo itakuwa na gharama za chini na yenye ufanisi.

Katika hotuba yake kupitia televisheni, rais pia alimfuta kazi mwanasheria mkuu lakini akamsaza waziri mwandamizi wa masuala ya kigeni Musalia Mudavadi na makamu wake wa rais Rigathi Gachagua akisisitiza kwamba serikali yake itaongozwa na makatibu wa kudumu katika wizara hizo.

Hatua yake ilifuatia maandamano ya hivi majuzi ya kupinga ongezeko la kodi na utawala mbaya .

Ruto anasema alichukua uamuzi huo baada ya kuwasikiliza wananchi na kwamba ataunda serikali pana baada ya mashauriano.

Lakini je rais Ruto alikuwa na chaguo jingine? Ni nini haswa kilichomshinikiza kulivunja baraza la mawaziri?

Kenya imeshuhudia machafuko ya wiki tatu ambapo waandamanaji walivamia bunge Juni 25 baada ya muswada wa fedha uliopendekeza nyongeza ya kodi kupitishwa.

Muswada huo ulikuwa ukiwaongezea kodi Wakenya licha ya kodi ya nyumba ya 1.5% iliowekwa awali na ile ya bima ya matibabu ya 2.7% ambayo bado haijatekelezwa.

Kulingana na mashirika ya kutete haki za binadamu, zaidi ya watu 41 waliuawa katika maandamano hayo , ambayo yamebadilika na kuwa wito wa kumtaka rais ajiuzulu.

Uvamizi huo wa bunge ambao ni wa kwanza katika historia ya taifa la Kenya na ambao ulisababisha uharibifu mkubwa uliwashangaza wengi sio tu hapa nchini bali Afrika na kote duniani.

Hata hivyo Rais aliutupilia mbali muswada huo kufuatia shinikizo hizo za vijana wa Gen Z ambao pia walimtaka kuwaachilia wenzao waliotekwa nyara mbali na kuzifidia familia za wenzao waliouawa katika maandamano hayo.

Na kufuatia wito huo rais aliitisha kikao na viongozi wa vijana hao ambao hadi sasa wamesema kwamba hawana kiongozi.

Wito huo uliambulia patupu huku vijana hao wakimtaka rais kufanya kikao nao katika mtandao wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter.

Katika kikao hicho ilibainika wazi kwamba vijana hao hawakukubaliana na masuala ambayo yaliangaziwa na rais huku mara nyengine wakisikika kukashifiana baada ya madai kwamba baadhi ya wenzao walikuwa wakishirikiana na serikali.

Utajiri wa ghafla wa baadhi ya viongozi wa serikali

Hivi majuzi baraza la wazee nchini Kenya liliunga mkono maandamano ya vijana wa Gen Z likimtaka rais William Ruto kukabiliana na ufisadi uliokithiri katika serikali yake.

Wazee hao waliomba uwajibikaji katika serikali wakitaka kujua jinsi baadhi ya viongozi wamekuwa matajiri ghafla na kutangaza utajiri wao hadharani.

“Tumeona watu waliokaa madarakani kwa muda usiozidi miaka miwili wakiwa na mamilioni ya fedha, wakitumia ndege kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine mbali na kutoa michango ya mamilioni ya hela kila wikendi katika harambee bila kujali vijana ambao hawana ajira,’’ walisema.

Hivi majuzi mmoja ya wabunge kutoka eneo la Bonde la Ufa ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Ruto alionekana akitoa mchango wa mamilioni ya fedha katika harambee.

Vile vile Waziri mmoja wa serikali yake pia alinukuliwa akisema kwamba saa yake aliovaa ilikuwa ikigharimu zaidi ya shilingi laki nane za Kenya. Hali hiyo ilizua ghadhabu miongoni mwa Wakenya waliotaka kujua ni wapi wawili hao walijipatia fedha hizo miaka miwili tu baada ya serikali ya Kenya kwanza kuchukua madaraka.

Raia wengi wamekuwa wakilalama kwamba serikali imekuwa ikikusanya kodi bila kuonesha ni wapi fedha hizo zimekuwa zikitumika .

Haya yanajiri licha ya madai ya serikali kwamba ilipata hazina ya serikali ikiwa tupu ilipochukua madaraka.

Katika siku za hivi karibu rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua wamekuwa wakilumbana, baada ya naibu huyo kutafuta uungwaji mkono katika eneo analotoka la mlima Kenya.

Eneo la Mlima Kenya lilitoa kura nyingi zilizomsadia rais Ruto kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2022.

Ili kuhakikisha kwamba eneo hilo linazungumza kwa kauli moja, naibu huyo wa rais amekuwa akitaka ushirikiano na aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa raia Ruto kabla na hata baada ya kampeni za uchaguzi wa 2022. Mpango huo wa Gachagua umevutia pingamizi kutoka kwa wandani wa rais Ruto ambao wameitaja kuwa ya ukabila.

Hali hiyo imezua mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho na kusababisha naibu wa rais kukosa usafiri katika hafla kadhaa za serikali.

Wakati Rais Ruto amekaa kimya kuhusu mvutano huo unaoongezeka, uamuzi wake wa kumkabili naibu wake kwa kuwa na maoni tofauti unaweza kuharibu ushirikiano wao wa kisiasa.

Vile vile mkuu wa Sheria katika serikali ya Kenya Justin Muturi amekuwa akilalamika kwamba serikali inafanya maamuzi bila kumshauri au kutozingatia ushauri wake.

Justin Muturi ambaye ndiye mshauri wa serikali kisheria anadai kwamba ushauri wake umekuwa ukipuuzwa kwa sababu za kimaslahi.