Bilionea wa Afrika Kusini ampiku Dangote kama mtu tajiri zaidi barani Afrika

Utajiri wa bwana Dangote umepungua kwa $1.7bn (£1.3bn) mwaka huu, na kufikia $13.4bn, Bloomberg inaripoti.

Muhtasari

•Bw Rupert anadhibiti Richemont, mojawapo ya makampuni makubwa zaidi ya bidhaa za anasa duniani, ambayo inamiliki chapa kama vile Cartier na Montblanc.

•Thamani yake imepanda kwa $1.9bn hadi $14.3bn, na kumfanya kuwa katika nafasi ya 147 duniani, nafasi 12 mbele ya Bw Dangote

Image: BBC

Bilionea wa Afrika Kusini Johann Rupert amempiku mfanyabiashara wa viwanda kutoka Nigeria Aliko Dangote kama mtu tajiri zaidi barani Afrika, kulingana na data ya hivi karibuni kutoka kwa Bloomberg Billionaires Index.

Bw Rupert anadhibiti Richemont, mojawapo ya makampuni makubwa zaidi ya bidhaa za anasa duniani, ambayo inamiliki chapa kama vile Cartier na Montblanc.

Thamani yake imepanda kwa $1.9bn hadi $14.3bn, na kumfanya kuwa katika nafasi ya 147 duniani, nafasi 12 mbele ya Bw Dangote.

Utajiri wa bwana Dangote umepungua kwa $1.7bn (£1.3bn) mwaka huu, na kufikia $13.4bn, Bloomberg inaripoti.

Kushuka kwa utajiri wa Bw Dangote kunadhihirisha mazingira magumu ya kiuchumi ya Nigeria, ambapo kampuni zake zinaendesha shughuli zake.

Tangu Rais Bola Tinubu ashike madaraka mwaka jana, ameanzisha mabadiliko kadhaa ya kiuchumi katika taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta, ambayo imechangia mfumuko mkubwa wa bei, ambao kwa sasa ni zaidi ya 30%.

Bw Tinubu alisema mabadiliko hayo ni muhimu ili kupunguza matumizi ya serikali na kuchochea ukuaji wa muda mrefu.

Kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya naira kumemuathiri pakubwa Bw Dangote, ambaye utajiri wake unahusishwa kwa kiasi kikubwa na mali zinazotumiwa katika sarafu ya nchi hiyo.

Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 66 alijipatia utajiri wake katika viwanda vya saruji na sukari - na mwaka jana alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta katika kitovu cha kiuchumi cha Nigeria, Lagos.

Himaya yake ya biashara, Kundi la Dangote, pia limekabiliwa na matatizo mengi katika miezi ya hivi karibuni kutokana na kucheleweshwa kwa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa .

Aliorodheshwa na jarida la Forbes mwezi Januari kama mtu tajiri zaidi barani Afrika kwa mwaka wa 13 mfululizo licha ya matatizo ya kiuchumi nchini humo.

Lakini ripoti ya hivi punde ya Bloomberg inamweka nafasi ya pili barani Afrika na ya 159 duniani.