Maelezo kuhusu shule ya Nyeri ambapo wanafunzi 17 walifariki katika kisa cha moto

Hillside Endarasha Academy ni shule ya msingi ya wasichana kwa wavulana iliyoko Kieni Magharibi, katika Kaunti ya Nyeri.

Muhtasari

•Katika taarifa yake, wizara ya elimu imebainisha kuwa shule hiyo ina wanafunzi 824, wavulana wakiwa 402 na wengine 422 wakiwa wasichana.

•Kipsang alithibitisha kwamba wavulana wote 156 wa bweni walikuwa wakilala katika jumba ambalo liliteketea.

ambapo wanafunzi 17 walifariki katika kisa cha moto mnamo Septemba 17, 2024.
Hillside Endarasha Academy ambapo wanafunzi 17 walifariki katika kisa cha moto mnamo Septemba 17, 2024.
Image: Wangare Mwangi// KNA

Nchi imeendelea kuomboleza baada ya wanafunzi kumi na saba kufariki na wengine kadhaa kujeruhiwa katika kisa cha moto kilichotokea katika shule ya Hillside Endarasha Academy iliyo eneo la Kieni, Kaunti ya Nyeri.

Kisa hicho kilichotokea Alhamisi usiku wa manane kimewaacha wengi katika hali ya huzuni huku wakizifariji familia za waathiriwa wa mkasa huo wa moto.

Wizara ya Elimu, katika taarifa yake Ijumaa asubuhi, imethibitisha kuwa wanafunzi 17 walipoteza maisha huku wengine 14 wakiachwa na majeraha.

Hillside Endarasha Academy ni shule ya msingi ya wasichana kwa wavulana iliyoko Kieni Magharibi, katika Kaunti ya Nyeri.

Katika taarifa yake, wizara ya elimu imebainisha kuwa shule hiyo ina wanafunzi 824, wavulana wakiwa 402 na wengine 422 wakiwa wasichana.

"Kati ya wanafunzi 824, wavulana 156 na wasichana 160 ni wa bweni, wakati wengine ni wasomi wa kutwa," PS wa Elimu ya Msingi, Belio Kipsang, alisema katika taarifa hiyo.

Kipsang alithibitisha kwamba wavulana wote 156 wa bweni walikuwa wakilala katika jumba ambalo liliteketea katika moto wa Alhamisi usiku.

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura alibainisha katika taarifa yake kuwa bweni hilo lilikuwa na wanafunzi wa darasa la 4–8.

Pia alithibitisha kuwa wanafunzi waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Mathari na Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyeri kupokea matibabu.

"Serikali imejitolea kikamilifu kusaidia waathiriwa, familia zao, na jamii pana ya shule katika wakati huu mgumu sana. Tunafanya kazi kwa karibu na mashirika yote husika, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, Shirika la Msalaba Mwekundu, na washikadau wengine wakuu, ili kutoa usaidizi unaohitajika,” Mwaura alisema.

Pia alithibitisha kuwa misaada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vyakula vikavu, matandiko, vifaa vya tiba, vifaa vya huduma ya kwanza na huduma za ushauri nasaha vimepelekwa shuleni hapo.

Siku ya Ijumaa asubuhi, Wakenya waliamkia habari za kusikitisha za mkasa wa moto ambao ulikuwa umegharimu maisha ya takriban wanafunzi 17 katika shule ya msingi ya kibinafsi katika Kaunti ya Nyeri.

Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua tayari wametuma risala zao za rambirambi kwa familia hizo na kuomba uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hilo.