Equatorial Guinea, nchi iliyoko Pwani ya Magharibi ya Ukanda wa Afrika ya Kati imekuwa ikivuma kwenye mitandao ya kijamii kwa zaidi ya saa 24 zilizopita.
Nchi hiyo yenye idadi ndogo ya watu ya chini ya milioni mbili iligonga vichwa vya habari kote duniani mnamo siku ya Jumatatu jioni baada ya mfanyibiashara na mwanasiasa mmmoja kudaiwa kunaswa katika kashfa ya ngono iliyohusisha wanawake wengi.
Bw Baltasar Ebang Engonga, anayeongoza Shirika la Kitaifa la Uchunguzi wa Kifedha (ANIF), anawajibika na kukabiliana na uhalifu wa kifedha na ufisadi.
Lakini katika hali ya kushangaza, sasa anakabiliwa na shutuma za kuhusika katika kashfa ya kanda za kimapenzi zinazodaiwa kuhusisha mamia ya rekodi za faragha.
Kulingana na ripoti, Engonga alirekodi kwa siri zaidi ya video 400 za maudhui chafu ambazo zinadaiwa kuwa na watu mashuhuri na wanafamilia wao, wakiwemo watu wa karibu sana na wasomi wa kisiasa wa Equatorial Guinea.
Inasemekana kuwa video hizi ni pamoja na wake, dada, na binamu za watu mashuhuri, na kufanya hii kuwa moja ya kashfa kubwa kukumba nchi katika kumbukumbu za hivi karibuni.
Kashfa hii imetikisa duru za kisiasa za Equatorial Guinea, ambapo faragha na uaminifu vinathaminiwa sana.
Engonga ana uhusiano mzuri ndani ya serikali na hata ana uhusiano na rais, jambo ambalo linafanya shutuma hizi kuwa za kushangaza. Watu wengi sasa wanatilia shaka uadilifu wa walio madarakani, wakijiuliza iwapo viongozi wanaotekeleza sheria na kupambana na uhalifu pia wanakiuka mipaka ya kimaadili.
Hapa chini kuna maelezo kadhaa kuhusu Equitorial Guinea ambayo unahitaji kujua: -
• Iko katika Afrika ya Kati.
• Mji mkuu ni Malabo.
• Ina ukubwa wa 28,000Km2
• Ina idadi ya watu milioni 1.8
• Ilipata uhuru kutoka kwa Wahispania, Oktoba 1968.
• Rais Teodoro Obiang ametawala tangu 1979.
• Ni moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta Afrika.
• Lugha kuu rasmi ni Kihispania.
•Raia wengi ni Wabantu.
• Dini kuu ni Ukristo.
• Ina kiwango cha juu zaidi cha kusoma na kuandika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.