Huenda doa limeingia katika uwaniaji wa Doris Petra na
mgombea mwenza Nick Mwendwa kuwania kiti cha urais katika shirikisho la soka
nchini FKF kwenye uchaguzi utakaoandaliwa Disemba 7 mwaka huu.
Mwendwa na Petra wamekuwa uongozini kwenye shirikisho hilo
kama rais na naibu mtawalia kwa zaidi ya miaka minane tangu kuchaguliwa kwao
wakihudumu mihula miwili. Mara hii tena, Nick Mwedwa analenga kusalia katika
nafasi ya pili ya juu zaidi katika FKF akilenga unaibu wa urais chini ya Doris
Petra anayewania urais. Hii ndio tuseme ni nipe nikupe ya kubadilishana wadhfa
tu.
Saa zinazidi kuyoyoma na siku zinakwenda kasi ikisalia takribani
mwezi mmoja kufikia uchaguzi wa FKF utakaondaliwa katika majimbo 48 (jimbo la
Nairobi limegawanywa uwili) kote nchini unaotazamiwa sana na washikadau wa soka
nchini. Wagombea wanazidi kushawishi wajumbe na vilabu kuwachagua wakiahidi
mazuri na marekebisho katika sekta ya soka nchini ikiwa watachaguliwa kuongoza
sekta hiyo yenye ufuasi mkubwa zaidi.
Kwa mujibu wa katiba ya shirikisho la soka nchini ya mwaka
2017 kifungu cha 37(e) katiba inasema kuwa muhila wa rais wa FKF na kamati kuu
ya kitaifa ni miaka mine na mamlaka yao yataanza rasmi baada ya kukamilika kwa
mkutano mkuu wa uchaguzi wa FKF. Katika kifungu hicho ibara ya (f) katiba hiyo
inatoa mwelekeo kuwa wanachama wote waliochaguliwa watahudumu kwa muda usiozidi
mihula miwili ikimaanisha kuwa mwanachama anaweza kuchaguliwa tena katika
nafasi nyingine na itahesabika kuwa muhula mpya katika ofisi atakayochaguliwa.
Kutokana na kifungo hicho cha 37(f), Nick Mwendwa na Doris
Petra wanapata fursa ya kuingia uchaguzini na kuomba fursa ya kuchaguliwa tena
kwa wadhfa tofauti waliokuwa wakihudumu kabla. Ila, huenda maji yakazidi unga
raundi hii baada ya waziri wa michezo Kipchumba Murkomen kutilia shaka uwaniaji
wa Petra na Mwendwa.
Awali bodi ya uchaguzi ya FKF iliyoteuliwa miezi michache
iliyopita iliwaidhinisha wagombea tisa kuwania urais wa FKF ikiwemo nibu rais
wa sasa Doris Petra na mgombea mwenza wake ambaye ndiye rais anayeondoka Nick
Mwendwa.
Akiwa mbele ya kamati ya michezo na utamaduni ya bunge la
kitaifa mnamo Jumanne 5, waziri Kipchumba Murkomen alitilia shaka hatua ya bodi
ya uchaguzi wa FKF kuidhinisha Nick Mwendwa kushiriki uchaguzi wa FKF kama
mgombea mwenza wa Petra.
Kulingana na waziri Murkomen, Nick Mwendwa amehudumu mihula
miwili tayari na kwa mujibu wa sheria rais huyo anayeondoka hastahili kuwania
tena unaibu rais wa FKF.
Murkomen ameitaka kamati hiyo ya bunge ya michezo na
utamaduni kuwajibisha bodi ya michezo ya FKF inayoongozwa na Hesborn Owilla
kama mwenyekiti na Merceline Sande kama katibu mkuu kutoa maelezo zaidi ya jinsi Nick Mwendwa
aliidhinishwa kuwania nafasi hiyo.
Aidha waziri Murkomen alijitenga na kutumia nguvu chini ya
ofisi yake kubandua bodi ya uchaguzi wa FKF akisema hiyo ni hatua ya mwisho zaidi
ikiwa hakuna kingine ambacho kitatekelezwa na washikadau husika kuhusiana na
kuidhinishwa kwa Mwendwa.
“Uamuzi wa waziri kuvunja timu yoyote ambayo imeanzishwa kinyume na
sheria upo, lakini tusiende mkondo huo, ni hatua ya mwisho. Naomba tufanye kazi
pamoja ili kupata mbinu mwafaka ya kuhakikisha uchaguzi wa huru na haki.” Alisema Murkomen.
Uchaguzi wa FKF huandaliwa kwa awamu tatu. Awamu ya kwanza
hufanyika katika kaunti kisha katika kitaifa na kukamilika katika kaunti ndogo
kote nchini.