Bila shaka lazima umeona jezi za timu zinazoshiriki ligi kuu
nchini Uingereza zikiwa na umbo la nambari nane yenye rangi ya nyekundu kifuani.
Umbo hilo ama niseme ua hilo linaitwa ‘Poppy’. ‘Poppy’ ni ishara ya ukumbusho
na matumaini katika mpira wa miguu ambayo inavaliwa kuwakumbuka watu waliokufa
vitani.
‘Poppy’ pia, kwa
wapenzi wa soka wameiona ikiwekwa uwanjani kabla ya mechi kung’oa nanga, kikosi
cha jeshi la Uingereza kikipiga tarumbeta sawia wakiwa wamebeba shada la maua.
Naam, kila msimu ligi ya primia, chama cha kandanda(FA),
ligi ya soka kwa ushirikiano na baraza la Uingereza ambalo ni shirika
linaloangazia utamaduni na elimu ya kimataifa nchini humo hushirikiana
kuadhimisha matukio muhimu yaliyotukia wakati wa vita vya kwanza vya dunia vya
mwaka 1914 tukio la msingi likiwa kumbukumbu ya mechi ya maridhiano maarufu kama ‘the 1914 Christmas Truce football match’.
Maadhimisho hayo ya Football Remembers yaliasisiwa mwaka wa
2014 baada ya washiriki mbali mbali kuanzisha elimu kuhusu matukio ya vita vya kwanza vya dunia
katika zaidi za shule na vituo vya mafunzo elfu thelathini katika nchini ya
Uingereza. Sababu kuu ya kuanzishwa elimu hiyo, ilikuwa kuwahamasisha kizazi
cha sasa na kijacho kuhusu umuhimu wa kandanda katika juhudi za kuleta amani wakipigia
mfano uelewano ulioafikiwa baina ya maadui wakati wa vita hivyo.
Kwa mujibu wa elimu inayotolewa kwa watoto wa Uingereza kuhusu
vita vya dunia vya kwanza, kupitia elimu hiyo, rasilimali zinatolewa kwa
wanafunzi ili kuwasaidia kuelewa zaidi.
Katika msimu huu wa 2024/2025, maadhimisho ya Football Remembers
yalifanyika Jumapili Novemba 10, vilabu mbali mbali vikiadhimisha siku hiyo kwa
kukumbuka wanajeshi mbali mbali na wachezaji wa soka waliofariki katika ukatili
wa vita hivyo.
Katika mechi ya Jumapili, ya Chelsea dhidi ya Arsenal ugani
Stamford Bridge ambayo ilikamilika kwa kufungana bao moja kwa moja, kabla ya
mechi, kulikuwepo na kimya cha sekunde kadhaa ili kuwakumbuka binadamu walioaga
dunia kupitia migorogoro mbali mbali kote duniani.
Dunia imeshuhudia migorogoro na vita ambavyo maelfu ya
watuwameuliwa ikiwemo vita vinavyoendelea
katika ukanda wa mashariki ya kati ikihusisha taifa la Israel na wanamgambo wa
Hezbollah katika eneo la Gaza vita ambavyo pia Lebanon imejipata ndani. Vile
vile vita kati ya Ukraine na Russia bila kusahau vita vya wenyewe kwa wenyewe
nchini Sudan.
Akizungumza kabla ya mechi hiyo nahodha wa Chelsea Reece James
alisema kuwa maadhimisho yao msimu huu katika klabu ya Chelsea kwa timu zote za
kiume na kike zililenga kuisadia jeshi la kifalme la Uingereza katika kupokea msaada
wa kuwaisaidia wale ambao wameishi na makovu ya vita.
Kauli mbiu ya jeshi la Kifalme ya Uingereza ya mwaka huu
ilikuwa kwamba mchango wa msamaria mwema unaweza kufanya mambo ambayo vifaa vya
kijeshi haviwezi kufanya.
Katika klabu ya Manchester United, timu hiyo iliadhimisha
siku ya Football Remembers kwa kukumbuka wachezaji wa zamani wa klabu hiyo waliopoteza maisha
yao kupitia makovu ya vita.
Katika makumbusho ya Manchester United ndani ya Old
Trafford, klabu hiyo ilikumbuka wachezaji wake wa zamani ikiwemo Gilbert
Godsmark aliyekuwa dereva katika jeshi na ambaye aliaga katika vita vya Boer
akihudumia jeshi la Newton Heath.
Kwenye makumbusho hayo ya Manchester United, baadhi ya
wachezaji waliowahi kuichezea klabu hiyo kisha wakaaga kutokana na vita vya
kwanza vya dunia walikumbukwa pia. Mchezaji Arthur Beadsworth ambaye alichezea
Man United pindi tu baada ya kubalishwa jina na kuwa Manchester United katika
msimu wa 1902/03 alikumbukwa pia. Arthur Beadsworth alikuwa sajenti katika
kikosi cha saba cha jeshi la Leicestershire.
Wengine ni Thomas Cliffford, wakikosi cha sita
na saba cha jeshi la Battalion Royal Scots Fusiliers, Benard Donaghey
aliyechezea Man United katika msimu wa 1905/06, George Elmore aliyechezea klabu
hiyo mwaka wa 1902, Hugh S. Kerr(1904), Harry Levis(1913/14), Oscar H.S Linkson
(1908/13), Patrick McGuire(1910/11), Harry Reynolds(1907-08) na Alexander ‘Sandy’
Turnbull (1906-15).