Mbunge wa eneo la Githunguri Peninnah Gathoni Muchomba amefunguka kuhusu azma yake kubwa ya kisiasa.
Akizungumza wakati wa mahojiano ya moja kwa moja na mwanahabari Samuel Maina, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alifichua kuwa ana ndoto ya kutwaa kiti cha juu zaidi nchini siku moja.
Alipoulizwa kama ana mipango mikubwa zaidi ya kisiasa kwa siku zijazo, alisema;
"Ni kweli nina mipango mikubwa zaidi, nina ndoto ya kuwa Rais wa Kenya siku moja."
Huku akizungumzia zaidi taaluma yake, mwakilishi wa kike huyo wa zamani wa kaunti ya Kiambu alibainisha kuwa angeendelea na kazi yake kama mtangazaji wa redio ikiwa hangejitosa katika siasa
Gathoni aidha alidokeza kuwa bado anapenda kazi yake ya awali ya utangazaji, akidokeza kwamba wakati atakapozeeka na kustaafu siasa bado ataendelea na kazi hiyo ambayo aliisimamisha kwa muda.
"Kama singekuwa mwanasiasa, labda ningeendelea na kazi yangu kama mtangazaji wa redio. Nilipenda maikrofoni sana, na nadhani hata ninapostaafu, wakati nikiwa nyanya bado nitakuwa nafanya podikasti,” alisema.
Aliongeza, "Ningependa kurudi kwenye media."
Gathoni pia alizungumza kuhusu mapenzi yake makubwa ya vitabu akibainisha kuwa yeye hutumia muda wake mwingi wa burudani kusoma.
"Ninapenda kusoma kuhusu harakati za wanawake wa Amerika kama vuguvugu la Suffragettes, vuguvugu la haki za kijamii kuhusu masuala ya wanawake kama vile harakati za miaka ya 1900. Nina maktaba kubwa ya vitabu vingi sana vilivyoandikwa kuhusu wanawake wazuri,” alisema.
Mama huyo wa watoto wawili alimtambua mume wake Robert Mbugua kama msukumo wake mkubwa zaidi maishani.
Pia alitaja wakati alipokuwa mke na hatimaye kuwa mama kama wakati wa kujivunia zaidi maishani mwake.
“Kuwa mama na kuwa mke kwa kweli hunipa uradhi mwingi,” alisema.
Gathoni alijitambulisha kama mama mkali.
Mbunge huyo pia hakusahau kutaja uhusiano wake wa karibu na bintiye na kufichua kuwa yeye ndiye mtu anayewasiliana naye zaidi kwenye simu.