Naibu Rais aliyetimuliwa Geoffrey Rigathi Gachagua amefunguka kuhusu maisha tangu kuondolewa kwake ofisini mnamo Oktoba 2024.
Akizungumza wakati wa mahojiano kwenye Inooro TV siku ya Jumapili usiku, Gachagua alisema kuondoka kwake ofisini kumempa amani na kumwezesha kuungana tena na wapendwa wake.
Gachagua pia aliangazia safari yake na kuangazia matukio tangu kuondoka ofisini.
"Nina amani sana na ninamshukuru Mungu kwa uhai na afya njema. Sasa nina muda wa kutafakari tumetoka wapi, tunaenda wapi na mambo yanaendeleaje," Gachagua alisema.
Naibu rais huyo wa zamani alisema kuwa mabadiliko hayo yamemwezesha kuwa na muda wa kufanya mazungumzo mazuri na marafiki na familia, jambo ambalo mara nyingi hangeweza kufanya hapo awali kwa sababu ya majukumu yake mengi kama naibu wa rais.
"Pia nina furaha kwa sababu sasa nina muda mwingi wa kuwasiliana na marafiki zangu, kufanya mazungumzo, na kuwatembelea watu ambao sikuwa nakutana nao hapo awali. Ninaweza kuketi na jamaa zangu, wale niliokua nao, na tukazungumza,” alisema.
Gachagua pia alizungumzia wakati anaotumia sasa na familia yake ya karibu na furaha ya kuwa na uhusiano mzuri na mke na watoto wake.
"Sasa nina muda wa kukaa na mke wangu na watoto wangu. Tunazungumza, na ninaridhika. Sina tatizo na mtu yeyote."
Mwanasiasa huyo alisema baadhi ya watu walitarajia angejitenga baada ya kutimuliwa, lakini akasisitiza kwamba yeye ni mnusurika na ni kipindi tu cha maisha.
“Kuna watu walidhani baada ya kutoka madarakani ningebaki ndani bila kufanya lolote, hata kuzungumza na mtu, mimi ni mtu ambaye nimeona na kupitia mambo mengi, mimi ni mnusurika, nikifa na kufufuka,” alisema
Gachagua alikuwa naibu wa kwanza wa rais kubanduliwa katika historia ya Kenya.
Alitimuliwa kwa mara ya kwanza na Bunge la Kitaifa mnamo Oktoba 8, na mnamo Oktoba 17, Seneti ikaidhinisha kuondolewa kwake.