Lion Junior, mtoto wa mtangazaji wa Radio Jambo Cyrus Afune almaarufu Lion Deh, alizikwa siku ya Jumamosi Januari 11, 2025.
Mtoto huyo wa umri wa mwaka mmoja na nusu alizikwa katika nyumbani kwa Lion katika kijiji cha Eshiongo, eneo bunge la Khwisero, kaunti ya Kakamega.
Marafiki, jamaa na wafanyakazi wenza wa mtangazaji huyo wa kipindi cha Mbusi na Lion Teketeke wakijumuika na familia ili kuomboleza pamoja nao na kumpa mtoto huyo mazishi ya heshima.
Lion Junior aliaga dunia mnamo Januari 8, 2025 kufuatia majeraha aliyopata kichwani baada ya kuanguka kutoka kwenye sofa wakati akicheza ndani ya nyumba.
Madaktari walikuwa wamemlaza mtoto huyo mdogo katika chumba cha wagonjwa mahututi baada ya kumfanyia upasuaji wa kichwa kwa lengo la kumponya.
Kwa bahati mbaya, jeraha alilopata mtoto huyo kichwani liliathiri ubongo wake, na kuacha maisha yake chini ya mashine ya kusaidia maisha, kabla ya kuaga mnamo Januari 8 asubuhi.
Mungu ailaze roho ya Lion Jr pema peponi!!