logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Baba wa muuguzi aliyerekodi akikufa maji avunja kimya kuhusu kifo cha bintiye

Bw Nyabuto alisema aliona giza ghafla na kuangua kilio kikubwa baada ya kufahamishwa yaliyompata bintiye.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri21 August 2022 - 10:08

Muhtasari


•Nyabuto alisema alichukua mkopo ili bintiye aweze kufunga safari ya kuelekea Kanada kama ilivyokuwa ndoto yake.

•Nyabuto alisema tayari amekubali kuwa amepoteza bintiye na kuomba msaada ili mwili wa marehemu uweze kuletwa Kenya.

Bwana John Nyabuto amefunguka kuhusu kifo cha binti yake Hellen Kemuntoi

Baba wa muuguzi wa Kenya ,Hellen Wendy Kemunto, ambaye alikufa maji katika dimbwi la kuogelea nchini Kanada usiku wa Alhamisi hatimaye amejitokeza kuzungumzia kifo cha binti yake.

John Nyabuto amefichua kuwa Bi Helen, 24,  alikuwa mtoto wa kwanza katika  familia yake ya watoto sita na alikuwa tegemeo lake kubwa.

Amesema alihangaika sana  kumsomesha Hellen pamoja na ndugu zake watano kwani hakuwa na kipato kikubwa na alitegemea kilimo pekee.

"Hakuweza kuenda chuo kikuu. Alianza kufanya biashara kidogo kidogo hapa. Aliendelea hivo mpaka akawa na ndoto ya kuenda ng'ambo. Mimi niliona ni kama ndoto kwa sababu sina jamaa au rafiki yeyote wa kumsaidia," Bw Nyabuto aliambia Nation.

Alibainisha kuwa alichukua mkopo ili bintiye aweze kufunga safari ya kuelekea Kanada kama ilivyokuwa ndoto yake.

Hellen alihamia nchi hiyo ya Marekani mwaka wa 2018 na kuanza kufanya kazi na vilevile kuhudhuria madarasa ya uuguzi.

'Sasa alikuwa anafanya Diploma in Nursing. Wakati hayuko shuleni alikuwa anaenda kibarua anapata hela kidogo anapata karo. Hata nilimwambia akipata kidogo yenye imebaki akumbuke watoto wengine hapa. Alikuwa anapata kidogo ananitumia anasaidia kulipa karo ya wengine na mengine," Alisema.

Nyabuto alisema kuwa hatimaye Hellen aligeuka kuwa tegemeo lake kuu na wanawe wengine  wakati yeye alianza kulemewa.

Alisema hakuweza kuamini wakati alipopokea habari kuhusu kifo chake asubuhi ya Ijumaa.

"Nilikuwa naangalia WhatsApp nijue kama mtoto wangu alishinda vizuri. Hapo ndipo nilipata habari ati kuna habari mbaya kutoka  kwa rafiki yake huko ng'ambo,"

Akizungumza na SirVick TV, Bw Nyabuto alifichua kuwa aliona giza ghafla na kuangua kilio kikubwa baada ya kufahamishwa yaliyompata bintiye. Wanafamilia wengine na majirani pia walijumuika naye kulia baada ya kuwapasha habari hizo za kuhuzunisha.

Nyabuto alisema tayari amekubali kuwa amepoteza bintiye na kuomba msaada ili mwili wa marehemu uweze kuletwa Kenya  kwa ajili ya mazishi.

'Hata usiku sikulala, nilikuwa nawaza jinsi mwili utakavyofika hapa kwangu niuzike. Hiyo ndiyo shida ambayo niko nayo. Sijui gharama itakuwaje. Sijiwezi. Ndugu zangu pia hawajiwezi, kuna ndugu yangu ambaye pia aliaga," Alisema.

Hellen alifariki Alhamisi usiku, takriban dakika kumi tu baada ya kuanza kupeperusha kipindi cha moja kwa moja kwenye Facebook.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved