Fahamu kwa nini watu wafupi, vigugumizi hawakubaliwi kujiunga na KDF- Lt Jonah Mwangi

Ili mwanamume ajiunge na jeshi ni lazima awe futi 5.4 na zaidi ilhali wanawake wanatakiwa kuwa na urefu usiopungua futi 5.

Muhtasari

•Luteni Mwangi alifichua kuwa silaha zinazotumiwa na wanajeshi katika vita kwa kawaida huwa ni kubwa, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto kubwa kwa watu wafupi.

•Luteni Mwangi alibainisha kuwa kazi hiyo inahitaji mawasiliano mazuri, jambo ambalo linaweza kuwapa changamoto watu wenye tatizo la kuguguma.

wapokea Nishani za Huduma za Umoja wa Mataifa kwa mchango wao katika amani mnamo tarehe 6 Agosti.
Wanajeshi wa Kenya walio nchini DRC wapokea Nishani za Huduma za Umoja wa Mataifa kwa mchango wao katika amani mnamo tarehe 6 Agosti.
Image: FACEBOOK// KDF

Naibu Mkuu wa Majeshi wa Kenya Luteni Jenerali Jonah Mwangi amefichua ni kwa nini watu wafupi hawakubaliwi kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).

Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Citizen Jumatano jioni, Mwangi aliweka wazi kuwa ili mwanamume ajiunge na jeshi ni lazima awe na urefu wa futi 5.4 na zaidi ilhali wanawake wanatakiwa kuwa na urefu usiopungua futi tano.

Naibu Mkuu huyo wa KDF alibainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa watu walio chini ya futi tano kukosa kufikisha uzito unaohitajika katika vikosi.

"Ikiwa unakuja na uzito zaidi ya unavyopaswa kuwa, basi kupitia mafunzo utapungua," Mwangi alisema.

Pia alibainisha kuwa silaha zinazotumiwa na wanajeshi katika vita kwa kawaida huwa ni kubwa, jambo ambalo linaweza kuleta changamoto kubwa kwa watu wafupi.

“Silaha tulizonazo ni zaidi ya futi nne. Unaweza kufikiria wakati umesimama kwenye gwaride, au unaenda vitani na silaha uliyonayo ni ndefu kuliko wewe? itakuwaje. Hiyo ni changamoto kubwa,” alisema.

Aliongeza, “Kama wewe ni chini ya kilo 50, na wakati wa mafunzo utahitajika kubeba kati ya kilo 18-25, hiyo itakuwa nusu ya uzito wako au karibu robo tatu ya uzito wako, unaweza kufanya hivyo? Unapokaribia mwisho wa mafunzo utahitajika kubeba mizigo mizito zaidi ambayo inaweza kuwa kutoka 25-45. Huwezi kubeba uzito wako mwenyewe."

Mwangi pia alithibitisha kuwa vikosi havikubali watu vigugumizi.

Alibainisha kuwa kazi hiyo inahitaji mawasiliano mazuri, jambo ambalo lingewapa changamoto watu wenye tatizo la kuguguma.

"Mchakato huu ni wa ushindani sana na watu wanaogugumia hawafanyi kwa mapenzi yao, lakini hii si kazi kama kazi nyingine yoyote na inahitaji ujuzi mzuri wa mawasiliano, kama hilo linawezekana. Ikiwa tatizo la kuguguma ni kubwa kuliko inavyowezekan, na inabidi nikuelekeze kufanya kitu, basi nikafikiri unahitaji kuwa mzungumzaji mzuri,” alisema.

Usajili wa KDF ulianza nchi nzima mnamo Julai 28 na unatarajiwa kukamilika Agosti 20.