Muhoozi Kainerugaba: Mambo unayohitaji kujua kuhusu mwanawe Museveni aliyetishia kuteka Nairobi

Muhoozi ndiye Kamanda wa Majeshi ya nchi kavu ya Uganda.

Muhtasari

•Muhoozi Kainerugaba alichapisha msururu wa jumbe zilizowakera Wakenya wengi na kukosolewa vikali.

•Muhoozi aldai kwamba itamchukua yeye na jeshi lake chini ya wiki mbili kuchukua udhibiti wa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

Image: WILLIAM WANYOIKE

Siku ya Jumatatu mwanawe Rais wa Uganda Yoweri Museveni alikua gumzo mitandaoni baada ya kuchapisha jumbe tatanishi ambazo zililenga Kenya.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Muhoozi Kainerugaba alichapisha msururu wa jumbe zilizowakera Wakenya wengi na kukosolewa vikali.

Katika ujumbe wake wa kwanza, Muhoozi alimtaja aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kama “kakake mkubwa’ na kumlaumu kwa kukosa kuwania urais kwa muhula wa tatu, na kuongeza kuwa angeshinda uchaguzi kwa urahisi.

"Tatizo langu pekee na kaka yangu mkubwa ni kwamba hakugombea muhula wa tatu. Tungeshinda kirahisi," aliandika.

Mwanawe Museveni alizidi kuidhalilisha Katiba ya Kenya akisema Uhuru alipaswa kubadilisha katiba ili kusalia madarakani.

"Haha! Nawapenda jamaa zangu wa Kenya. Katiba? Utawala wa sheria? Lazima uwe unatania! Kwetu (Uganda), kuna Mapinduzi tu na muda si mrefu mtayafahamu!" alisema.

Muhoozi aliendelea kudai kwamba itamchukua yeye na jeshi lake chini ya wiki mbili kuchukua udhibiti wa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

"Haingetuchukua sisi, jeshi langu na mimi, wiki 2 kuteka Nairobi," alisema.

Wakenya waliokuwa wamejawa na ghadhabu walikita kambi kwenye akaunti ya Twitter ya Muhoozi na kujibu matamshi yake.

Je, huyu Muhoozi ni nani?

Hapa chini tunaangazia mambo 10 kuhusu mwanawe rais Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba:-

1. Ni mtoto wa kwanza wa rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.

2. Alizaliwa Aprili 24, 1974. Ana umri wa miaka 48.

3. Ni mume wa Charlotte Nankunda Kutesa kutoka 1999.

4. Ana watoto watatu.

5 Alijiunga na Jeshi ya Uganda mwaka wa 1999.

6. Mwaka wa 2011 alipandishwa cheo kuwa kanali.

7. Mwaka wa 2017 aliteuliwa kuwa mshauri mkuu wa rais kuhusu Majukumu maalum.

8. Mwaka wa 2019 aliteuliwa kuwa Luteni Kanali. 

9.Mwaka wa 2021 aliteuliwa kuwa Kamanda wa Majeshi ya nchi kavu ya Uganda.

10. Aliwahi kusomea Kenya katika shule ya msingi ya Mount Kenya Academy , Nyeri.