Muokoaji asimulia matukio ya kutisha katika eneo la ajali iliyowaua watu 34

Mtoto ambaye Gitonga alibeba alitangazwa kufariki alipofikishwa katika hospitalini.

Muhtasari

•Gitonga alisema  alipatwa na huzuni baada ya mtoto wa umri kama wa mwanawe kutangazwa kuwa amefariki alipofikishwa.

•Alisema ajali hiyo ilimkumbusha ajali ya basi la Tawfiq iliyotokea 1997, ambayo iliua zaidi ya watu 40 papo hapo.

Basi la Modern Coast latumbukia kwenye mto Nithi
Image: HISANI

Jumatatu idadi ya waliofariki kwenye ajali iliyotokea Jumapili katika daraja la Nithi iliongezeka hadi 34 huku waokoaji wa kwanza kufika katika eneo la ajali Jumapili jioni wakisimulia hali ya kutisha iliyokuwa pale.

Dereva wa basi la Modern Coast alishindwa kulidhibiti na kutumbukia mtoni kando ya barabara ya Meru-Nairobi.

Mutuiri Gitonga alikuwa miongoni mwa waliopambana kuokoa maisha baada ya ajali hiyo kutokea.

Alipigiwa simu na rafiki yake, Daizy Rutere, akimjulisha kuhusu ajali hiyo.

Gitonga alisema alipowasili magari na bodaboda nyingi tayari yalikuwa zilikuwa zimefunga barabara.

"Wakazi walikuwa wakiwabeba wahasiriwa juu ya bonde, kutoka kwa basi, ambalo lilikuwa limezama nusu," alisema.

Gitonga alisema ajali hiyo ilimkumbusha ajali ya basi la Tawfiq iliyotokea 1997, ambayo iliua zaidi ya watu 40 papo hapo.

Alisema alipatwa na kiwewe baada ya mtoto wa umri kama wa mwanawe kutangazwa kuwa amefariki alipofikishwa katika Hospitali Kuu ya Chuka.

“Nilimtoa mtoto kwenye msibani na kusimamisha taxi gari ili kutupeleka hospitalini. Nilikuwa nimembeba mtoto huku waathiriwa wengine wawili wakiwa nyuma ya gari,” Gitonga alisema.

Alisema akiwa njiani, alipiga simu hospitalini hapo ili wajiandae kumpokea mtoto huyo na kuanza matibabu ya dharura.

Mtoto huyo hata hivyo alitangazwa kufariki alipofikishwa katika hospitali ya Chuka.

Ingawa alihuzunika moyo, Gitonga alisema alirejea eneo la tukio kwa kutumia gari la polisi ambalo lilikuwa limeleta miili zaidi hospitalini.

Kufikia saa nne usikuwa wa  Jumapili polisi walisema miili 22 ilikuwa imekusanywa kutoka eneo la tukio huku wengine wakithibitishwa kufariki walipowasili hospitalini.

Walisema baadhi ya wagonjwa 13 walikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali za Chogoria na Chuka.

Walioshuhudia walisema basi hilo lililokuwa likielekea Mombasa lilikuwa likitoka mjini Meru wakati ajali hiyo ilipotokea.

Walisema dereva alishindwa kulidhibiti na kutumbukia mtoni.

Kikosi cha zimamoto na uokoaji cha Tharaka Nithi, Msalaba Mwekundu wa Kenya, maafisa wa polisi na wananchi walisaidia katika kazi ya uokoaji.

Kamishna wa Tharaka Nithi Nobert Komora alisema basi hilo la Modern Coast lilitoka Maua na kuhusisha ajali hiyo mbaya ya saa kumi na mbili na nusu usiku na kufeli kwa breki, kulingana na uthibitisho.

“Tunasikitika kuripoti kuwa tumepoteza watu 33. Wengine 13 ambao wako katika hali mbaya wanahudumiwa katika hospitali za Chogoria na Chuka," alisema.

Komora alisema basi lilihusika kwenye ajali lina uwezo wa kubeba takriban abiria 44.

"Tunahitaji kufahamu idadi ya watu waliokuwa wamepanda basi.

"Msako unaendelea chini ya mkondo na tumeanza uchukuaji wa mabaki ya mto huo. Pia tunasubiri kamati ya usalama ya mkoa inayoongozwa na kamishna Evans Achoki," alisema.

Madereva hata hivyo wameonywa kupunguza mwendo wanapofika  kwenye mteremko mkali wa Nithi. 

Nicholas Mutegi, mmoja wa walioshuhudia ajali, alisema basi hilo lilikuwa likishuka kwa kasi kwenye mteremko wa Nithi kabla ya ajali kutokea. "Liligonga nguzo za ulinzi na kuanguka ndani ya maji.

Nilisikia kishindo kikubwa lilipoanguka umbali wa mita 40 na kusababisha basi hilo kuwa mabaki, nilihesabu zaidi ya maiti 10 ambazo ziliwekwa kwenye gari la polisi huku zaidi ya 20 wakijeruhiwa." alisema.

Wakaazi waliitaka Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu na serikali za kitaifa na zile za kaunti kubuni upya barabara hiyo.

 Laban Karani alisema daraja la Nithi limekuwa kaburi wazi.

 "Tutapoteza maisha hadi lini kwa sababu ya ubovu wa usanifu wa barabara? Serikali ihamishe daraja au barabara ili kuzuia maafa yajayo.

Hakuna gharama ambayo inaweza kulinganishwa na maisha yaliyopotea tangu miaka ya 1980," alisema. 

Barabara hiyo  ina njia mbili za kupanda kuelekea Marima lakini njia moja tu ya Mitheru. 

Mwaka wa 1988, watu 50 walikufa kwenye daraja. Baadhi ya 158 walikuwa wameangamia kabla ya 2000.

(Utafsiri: Samuel Maina)