Familia moja inaomboleza kifo cha mtoto wao wa miezi tisa katika kituo cha kulelea watoto walichomuacha katika mtaa wa mabanda wa Kiambiu, Nairobi.
Wazazi wa mtoto huyo waliambia polisi kuwa walimwacha mvulana huyo kwa mwanamke ambaye anaendesha huduma za kulelea watoto mchana katika Biafra Alhamisi asubuhi ili kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kujikimu kimaisha.
Wazazi hao hufanya kazi za mikono katika eneo hilo ili kujipatia riziki.
Hii inawalazimu kumuacha mtoto katika kituo cha kulelea watoto ili kufanya kazi ya kupata mkate.
Walirudi mida ya saa kumi na moja jioni tayari kumchukua kijana huyo lakini wakamkuta amelala hoi.
Walimkimbiza katika Hospitali ya Mother and Child katika California ambako alitangazwa kuwa amefariki alipofika. Chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana.
Polisi walitembelea kituo hicho kama sehemu ya uchunguzi wa kifo.
Mwili ambao haukuwa na majeraha yoyote ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi na maiti, polisi walisema.
Katika eneo la Butere, Kaunti ya Kakamega, polisi wanachunguza mauaji ya mtoto wa miezi mitano.
Mama wa mtoto huyo alisema alikwenda kuchota maji na kumuacha mtoto akiwa amelala nyumbani.
Aliporudi alikuta mlango wake ukiwa wazi na alipoingia ndani alimkuta mtoto amelala chini amekufa.
Polisi walitembelea eneo la tukio na kubaini kuwa nyumba hiyo yenye vyumba viwili yenye kuta za udongo ilivunjwa na mtu asiyejulikana ambaye alimuua mtoto huyo.
Mwili ambao haukuwa na majeraha yoyote ulihamishwa hadi Butere Funeral Home ukisubiri uchunguzi wa maiti.