Mtuombee tafadhali! Mkewe Wafula Chebukati awasihi Wakenya

Mary Chebukati alifunguka jinsi kazi ya mumewe imemuweka mbali na familia yake.

Muhtasari

•"Saa zingine tunamwona kwa tv zaidi kuliko tunavyomwona nyumbani sababu ya hii kazi," Mary  alisema.

•Mary alibainisha kuwa wakati wa uchaguzi wa 2017 familia yao ilikuwa na wasiwasi mkubwa.

Mary Chebukati, mke wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati.
Mary Chebukati, mke wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati.
Image: HISANI

Huku zikiwa zimesalia siku 22 kufanyika kwa uchaguzi mkuu, Mke wa mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi na mipaka Wafula Chebukati amewataka wakenya kumuombea.

"Naomba tu mtuombee, mtuombee kama familia wakati huu wenye tunaingia uchaguzi huu, mimi naomba mtuombee sababu mimi najua mzee kitu kimoja anataka kufuata sheria."

Akiongea wakati wa ibada ya mazishi siku ya Jumamosi, Mary alifunguka jinsi kazi ya mumewe imemuweka mbali na familia yake.

"Saa zingine tunamwona kwa tv zaidi kuliko tunavyomwona nyumbani sababu ya hii kazi," alisema.

Alibainisha kuwa wakati wa uchaguzi uliopita familia yao ilikuwa na wasiwasi mkubwa lakini mwaka huu wana nguvu zaidi.

"Wakati wa ule uchaguzi mwingine watoto walikuwa na huzuni sana lakini sasa wako na nguvu na hata yeye mwenyewe ako na nguvu na kila siku tunamuombea tukisema Mungu ampatie hekima, Mungu muoshe na damu ya Yesu ili atumikie nchi hii."

Mnamo Januari 18, 2017 Rais Uhuru Kenyatta alimteua Chebukati kuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi akichukua hatamu kutoka kwa Issack Hassan.

 Akiwa na timu ya makamishna sita, Chebukati alisimamia uchaguzi Mkuu wa 2017 ambao ulikuwa na marudio ya uchaguzi wa urais mwezi Oktoba ambapo Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto walitangazwa washindi.

Kwa uchaguzi wa mwaka huu, Chebukati amekuwa chini ya shinikizo la kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki, uliotawaliwa na dosari zozote

(Utafsiri: Samuel Maina)