Mwanafunzi mmoja afariki, 33 wajeruhiwa katika ajali ya basi Kisumu

Wakati huo ndipo mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 17 alifariki papo hapo, walioshuhudia walisema.

Muhtasari
  • Polisi na maafisa kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama wanashiriki katika kampeni ya kukabiliana na tishio hilo barabarani.
lililohusika katika ajali.
Basi la Easy Coach lililohusika katika ajali.
Image: HISANI

Mwanafunzi mmoja alifariki huku takriban 33 wakijeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi lililokuwa limebeba wanafunzi wa shule ya upili ya Wavulana ya Chavakali mjini Kisumu.

Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga huko Kisumu kwa matibabu kufuatia ajali iliyotokea Jumatatu usiku katika Barabara Kuu ya Kisumu-Kakamega, polisi walisema.

Basi hilo lilikuwa likiwasafirisha wanafunzi hao kuelekea Nairobi kufuatia kufungwa kwa shule kwa muhula wa kwanza.

Kulingana na walioshuhudia, dereva alipoteza udhibiti katika mzunguko wa Mamboleo mjini Kisumu.

Alisema dereva alionekana kuwa na mazungumzo kwenye mzunguko wa barabara ndipo aliposhindwa kulidhibiti basi hilo na kugonga reli ya walinzi na kutua ukingo wa barabara.

Wakati huo ndipo mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 17 alifariki papo hapo, walioshuhudia walisema.

Mwangi alisema wanafunzi hao wengine walipata majeraha madogo na wako katika hali nzuri hospitalini.

“Wazazi na walezi wa baadhi ya wanafunzi wamefika na wanawahudumia. Wameumia lakini wako salama,” alisema.

Aliongeza wazazi wengine wengi walipiga simu kuangalia usalama wa wapendwa wao.

Wanafunzi hao waliokolewa kutoka eneo la tukio na gari la wagonjwa na wasamaria wema.

Haya yanajiri huku kukiwa na kampeni inayoendelea ya kukabiliana na ongezeko la visa vya ajali nchini.

Polisi na maafisa kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama wanashiriki katika kampeni ya kukabiliana na tishio hilo barabarani.

Zaidi ya watu 1,000 wamepoteza maisha katika ajali za barabarani tangu Januari mwaka huu.

Wengine wanauguza majeraha katika maeneo mbalimbali baada ya ajali hizo.

Hii inaweza kutoa dalili angalau watu 30 hufa kila siku katika ajali, maafisa walisema.

Hii imeziacha familia nyingi kuathirika vibaya. Ajali kama hizo zina athari mbaya kwa familia kwa ujumla.

Mwendo kasi ndio chanzo kikuu cha ajali za barabarani pamoja na kupishana, ulevi, uzembe na magari yasiyofaa barabarani.