Msanii wa kizazi kipya nchini Kenya, Willy Paul amezindua gari lake jipya ambalo limepambwa kwa njia ya kipekee.
Gari hilo ambalo ni la abiria kumi na nne Pozee, kama ambavyo anajiita kimajazi amesema lipo tayari kutumika na lipo wazi kwa watu kulikodisha kwa matumizi ya kibinafsi.
Katika picha mbali mbali ambazo Willy Paul amepakia kwenye mtandao wake wa Facebook, zinaonesha akiwa amechorwa kwenye gari pamoja na majina yake ya kimajazi kama Pozee, pamoja pia na jina la lebo yake ya Saldido.
Alidokeza kwamba huenda hiyo ndio biashara yake mpya ambayo ameanza, kuyapamba magari na kisha kuyakodisha kwa matumizi maalum.
“Fungua kuona gari langu jipya, biashara yangu mpya. Utukufu wote ni kwa Mungu. Lipo wazi kwa ajili ya kukodisha, kitu chenye haiba yake rafiki zangu,” Willy Paula aliandika.
Hapa tunakuandalia baadhi ya picha za gari hilo na jinsi lilivyopambwa kweli kweli.