Kiongozi wa Azimio Raila Odinga alitembelea familia ya marehemu Prof George Magoha Jumatano katika makazi ya Lavington jijini Nairobi.
Ziara yake ilikuja muda mfupi baada ya ziara kama hiyo ya mkurugenzi mtendaji wa Azimio Raphael Tuju.
Viongozi kadhaa wameendelea kukusanyika nyumbani ili kuwapa pole familia hiyo kutokana na msiba huo huku heshima zikiendelea kumiminika.
Magoha, 71, alifariki Jumanne jioni katika Hospitali ya Nairobi.
"Ni kwa masikitiko makubwa kwamba tunatangaza kifo cha ghafla na kisichotarajiwa cha Profesa George Magoha jioni hii katika Hospitali ya Nairobi," Mkurugenzi Mtendaji wa The Nairobi Hospital James Nyamongo alisema katika taarifa.
Magoha amemuacha mjane Babra Magoha na mwanawe mmoja Michael Magoha.
Bosi huyo wa ODM alisema mara ya mwisho walipowasiliana ilikuwa wiki mbili zilizopita walipozungumza kwa simu.
"Tumekuwa tukizungumza kwa simu, mara ya mwisho nilizungumza naye ni takriban wiki mbili zilizopita. Tulikuwa tunazungumza kuhusu mabadiliko, nadhani alikuwa ameenda kufanya mahojiano katika chuo kikuu cha Maseno," Raila alisema.