Rais Uhuru Kenyatta akemea ubaguzi katika utoaji wa chanjo duniani

Rais Kenyatta alisema kuwa licha ya watafiti wa Kenya kushiriki kikamilifu katika kutengeneza chanjo za AstraZeneca, bado kulikuwa na ukosefu wa vifaa vya uzalishaji nchini.

Muhtasari

•Rais Kenyatta alisema kuwa nchi yake imekumbana na changamoto ya utaifa kwanza katika utoaji wa chanjo

•Rais alisema sasa ni lengo lao kuhakikisha kwamba Kenya haiendelei kuwa mwathirika wa utaifa kwanza katika kupata chanjo ya Covid 19.

Image: IKULU KENYA

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amezungumza kuhusu changamoto ya ukosefu wa uwezo wa uzalishaji wa chanjo ya Covid-19 nchini humo.

Katika mahojiano na BBC, Rais Kenyatta pia alisema nchi yake imekumbana na changamoto ya utaifa kwanza katika utoaji wa chanjo.

Rais Kenyatta alisema kuwa licha ya watafiti wa Kenya kushiriki kikamilifu katika kutengeneza chanjo za AstraZeneca, bado kulikuwa na ukosefu wa vifaa vya uzalishaji nchini.

Rais alisema sasa ni lengo lao kuhakikisha kwamba Kenya haiendelei kuwa mwathirika wa utaifa kwanza katika kupata chanjo ya Covid 19.

Akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa Elimu ambao alishiriki kwa pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson huko London, Bw Kenyatta pia alisema alikuwa na furaha ya kuwekeza fedha zinazotolewa na Muungano wa Elimu Duniani.

Alisema hii itahakikisha kuwa wanafunzi walioathirika na mimba za umri mdogo na wale ambao waliacha shule kwasababu ya Covid-19 wanaandikishwa tena shuleni kumaliza masomo yao katika mfumo rasmi.