Jamaa auawa baada ya mwenye boma kurejea usiku na kumfumania akijiburudisha na mkewe Nakuru

Nyaberi alimdunga Njagi alipoomba aruhusiwe achukue viatu vyake ili aondoke.

Muhtasari

•Micah Nyaberi Bogomba, 39, alimshambulia Boniface Njagi Maina, 34 kwa kisu na kumuua papo hapo baada ya kumpata na mkewe Harriet Vivian Mboga mida ya saa tisa usiku.

•Hapo wanandoa hao wawili, Nyaberi na Vivian wakatiwa pingu na kufikishwa katika kituo cha polisi ili kutoa majibu kuhusu kifo cha Njagi

Crime scene
Crime scene

Ama kweli, wanamuziki wa bendi ya Sauti Sol hawakukosea walipoimba "..Bibi ya wenyewe is a  no go zone..!"

Kizaazaa kikubwa kiliibuka maeneo ya Kagoto kaunti ya Nakuru alfajiri ya Jumamosi baada ya  mwanaume mmoja kurejea nyumbani na kumpata jamaa akijistarehesha  na mkewe.

Micah Nyaberi Bogomba, 39, alimshambulia Boniface Njagi Maina, 34 kwa kisu na kumuua papo hapo baada ya kumpata na mkewe Harriet Vivian Mboga mida ya saa tisa usiku.

Nyaberi ambaye alikuwa ametoka safarini aliwapata wawili hao na huku akiwa amejawa na ghadhabu tele akadai kujua kilichokuwa kinaendelea.

Katika harakati ya kudai majibu, Nyaberi alimshambulia Njagi kwa ngumi na mateke kabla ya kuchukua kisu na kumdunga mgongoni.

Kulingana na DCI, Nyaberi alimdunga Njagi alipoomba aruhusiwe achukue viatu vyake ili aondoke.

Polisi kutoka kituo cha Kagoto walikimbia katika eneo la tukio na kupata mwili wa marehemu ukiwa umelalal juu ya dibwi la damu yake.

Katika eneo la tukio, maafisa wa polisi walipata damu nyingi ikiwa imetapakaa kila mahali kwenye nyumba.

Hapo wanandoa hao wawili, Nyaberi na Vivian wakatiwa pingu na kufikishwa katika kituo cha polisi ili kutoa majibu kuhusu kifo cha Njagi.