COVID 19: Wagonjwa 1967 wamelazwa hospitalini, Vifo 16 zaidi vyaripotiwa

Takriban wagonjwa 1247 wameripotiwa kupona ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita.

Muhtasari

•Tangu mwanzo wa janga la Corona mwaka uliopita Kenya imeandikisha visa 234, 952 kutoka kwa vipimo 2,363, 524 ambavyo vimeweza kufanywa.

Waziri Mutahi Kagwe
Waziri Mutahi Kagwe
Image: HISANI

Visa 363 zaidi vya waathiriwa wa virusi vya Corona vimeripotiwa nchini hivi leo. Jumla ya vipimo 4594 viliweza kufanyiwa nchini ndani ya kipindi cha masaa 24, kuashiria kuwa asilimia ya maambukizi nchini kwa sasa ni 7.9%.

Mtoto wa miaka miwili ndiye mdogo zaidi aliyepatikana na virusi vya Corona kwenye kipindi hicho huku mkongwe wa miaka 97 akiwa mzee zaidi kupatikana na virusi hivyo.

Tangu mwanzo wa janga la Corona mwaka uliopita Kenya imeandikisha visa 234, 952 kutoka kwa vipimo 2,363, 524 ambavyo vimeweza kufanywa.

Kaunti ya Nairobi ndiyo ameandikisha visa vingi leo ikiripoti wagonjwa 117 ikifuatwa kwa umbali na Kiambu ambayo imeandikisha visa 36. Nyeri na Uasin Gishu zinafuata zikiwa na visa 29 kila mmoja.

Takriban wagonjwa 1247 wameripotiwa kupona ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita. 1114 kati yao walikuwa wanahudumiwa manyumbani huku 113 wakiwa wameachiliwa kutoka vituo mbalimbali vya afya nchini.

Hata hivyo, vifo 16 zaidi vimeripotiwa na kufikisha idadi ya walioangamia kutokana na maradhi ya COVID 19 nchini kuwa 4,710.

Kwa sasa wagonjwa 1,967 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku wengine 6,959 wakiendelea kuhudumiwa manyumbani. Wagonjwa 159 wamelazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi.

Chanjo ya Corona.

Kufikia sasa angalau watu 1,939,688 wameweza kupokea angalau dozi moja ya chanjo dhidi ya Corona huku 802,511 kati yao wakiwa wamepokea dozi zote mbili.