Jamaa achoma sehemu za siri za mkewe na chai moto baada ya kumpata akisoma ujumbe aliotumiwa na mwanadada kwa simu yake

Mama huyo wa watoto watatu ambaye alionekana kulemewa kutembea vizuri aliugua majeraha mabaya sio tu kwenye sehemu za siri mbali pia kwenye mapaja yake.

Muhtasari

‚ÄĘSharon Chepkorir, 25, amesema kuwa mumewe Alfred Kigen, 32,  aliingia na kumpata akiandika nambari ya aliyekuwa ametuma ujumbe huo uliosoma "Mambo" na hapo ndipo akaendea chai iliyokuwa inaiva jikoni na kuimwaga kwenye sehemu zake za siri.

crime scene
crime scene

Jamaa mmoja kutoka kijiji cha Kapsir katika kaunti ya Bomet anaripotiwa kuchoma sehemu za siri za mkewe kwa chai moto baada ya kumpata akisoma ujumbe wa simu ambao ulikuwa umetumwa na mwanadada mwingine kwa simu yake. 

Sharon Chepkorir, 25, amesema kuwa mumewe Alfred Kigen, 32,  aliingia na kumpata akiandika nambari ya aliyekuwa ametuma ujumbe huo uliosoma "Mambo" na hapo ndipo akaendea chai iliyokuwa inaiva jikoni na kuimwaga kwenye sehemu zake za siri.

"Nilikuwa nimeshika simu ya mzee nikapata ujumbe wa mtu mwingine nikachukua namba. Mzee wangu akanipata nikiwa natoa namba kwa simu yake. Alipoona namba ambayo nilikuwa nimeandika akaenda jikoni akatoa chai kwa moto alafu akanichoma nayo kwenye sehemu za siri. Saa hii hata siwezi kuenda msalani" Chepkorir alieleza wanahabari siku ya Jumapili akiwa nyumbani kwa wazazi wake ambako anaendelea kuponya majeraha.

Mama huyo wa watoto watatu ambaye alionekana kulemewa kutembea vizuri aliugua majeraha mabaya sio tu kwenye sehemu za siri mbali pia kwenye mapaja yake.

Mwanamke aliyekuwa amemtumia Kigen ujumbe ulioibua mzozo anadaiwa kuwa mpango wake wa kando.

Kulingana na familia ya Sharon, sio mara ya kwanza wanandoa hao wawili wamekuwa wakizozana na mara kwa mara ugomvi umeibuka kati yao. Wametoa ombi kwa serikali kuchukua hatua kali dhidi ya mshukiwa.