Mshtuko Nyeri baada ya jamaa kuua ndugu yake mkubwa kwa upanga kufuatia mzozo wa kiti

Muhtasari

• Maina alikuwa ametumwa na mama yao kuenda kwa ndugu yake mdogo kuchukua sofa ambayo alikuwa amechukua  wakati malumbano makali yaliibuka kati yao na vita ikaanza.

Crime scene
Crime scene

Hali ya mshtuko ilitanda katika eneo la Kamakwa kaunti ya Nyeri usiku wa Jumanne baada ya jamaa mmoja kuua ndugu  yake kwa upanga kufuatia mzozo uliohusisha kiti aina ya sofa.

Elias Muriithi Kariuki, 36, anaripotiwa kukata ndugu yake mkubwa Joseph Maina  kichwani kwa kutumia upanga mkali kabla ya kujisalimisha kwa polisi.

Kulingana na DCI, Maina alikuwa ametumwa na mama yao kuenda kwa ndugu yake mdogo kuchukua sofa ambayo alikuwa amechukua  wakati malumbano makali yaliibuka kati yao na vita ikaanza.

Wakati vita kati ya wawili hao ilikuwa imenoga, Muriithi anaripotiwa kuchukua upanga mkali kutoka kwa nyumba yake na kumkata ndugu yake mkubwa kichwani mara kadhaa na kumuacha akiwa hali mahututi.

Majirani walipokuwa wanafanya juhudi kujaribu kuokoa maisha ya Maina, Muriithi alifululiza moja kwa moja hadi kituo cha polisi cha Mathari na kujisalimisha kwa kuhofia kupigwa kitutu na wakazi waliokuwa wamejawa na ghadhabu.

Polisi walipofika kwenye eneo la tukio baada ya kupokea taarifa walipata mwili wa marehemu ukiwa umelala kwenye dibwi la damu yake.

Muriithi alikamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu mashtaka ya mauaji yanayomkabili.