Mshtuko Busia baada ya mwanadada kushirikiana na babake kutupa kitoto kidogo ndani ya choo

Muhtasari

•Butwaa kubwa iliwapata wanakijiji wakati vilio vikali vya kitoto hicho vilisikika kutoka ndani ya shimo la choo chenye kina cha futi 20  na hapo wakaarifu maafisa wa kulinda usalama.

•.Kulingana na chifu wa eneo la Asing'e Willimina Inyaa, kitoto kile kilipatikana kikiwa kimefungwa na majani ya ndizi huku kikiwa kimejawa na funza mwilini.

Image: ABSALOM NAMWALO

Habari na Absalom Namwalo

Polisi katika kaunti ya Busia wanazuilia mwanaume mmoja na binti yake kwa kosa la kutupa kitoto chenye uzani wa kilo 2.8 kwenye choo cha shimo.

Wawili hao wanadaiwa kushirikiana kutekeleza kitendo hicho cha unyama nyumbani kwao katika kijiji cha Asing'e eneo la Teso Kusini.

Msichana mhusika ambaye ni mwanafunzi wa mafunzo ya udaktari alikamatwa pamoja na baba yake ambaye ni mwalimu wa zamani ili kutoa habari zaidi kuhusiana na tukio hilo.

Butwaa kubwa iliwapata wanakijiji wakati vilio vikali vya kitoto hicho vilisikika kutoka ndani ya shimo la choo chenye kina cha futi 20  na hapo wakaarifu maafisa wa kulinda usalama.

Kwa neema zake Maulana kitoto kile kiliweza kuokolewa kutoka kwenye shimo hilo  na kukimbizwa hadi kituo cha matibabu cha Lukolis na baadae kuhamishwa kupelekwa hadi hospitali ya rufaa ya Busia kwa matibabu zaidi.

Kulingana na chifu wa eneo la Asing'e Willimina Inyaa, kitoto kile kilipatikana kikiwa kimefungwa na majani ya ndizi huku kikiwa kimejawa na funza mwilini.

Tukio hilo limeibua maswali mengi kuhusiana na ni nani baba ya kitoto kile na mbona hakikukaribishwa pale katika boma ile kuona kuwa baba na bintiye walishirikiana kupanga njama ya kukitupa.

Uchunguzi ungali unaendelea huku washukiwa wakitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya wapelelezi kukamilisha ripoti yao.