Mwanafunzi wa kidato cha pili ajitia kitanzi ndani ya nyumba ya mpenzi wake Bungoma

Muhtasari

•Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na jamaa ambaye ni mjenzi katika mjengo unaoendelea katika eneo lile.

meru
meru

Huzuni imetanda katika eneo la Kabula kaunti ya Bungoma baada ya mwanafuzi wa kidato cha pili kujitia kitanzi kufuatia kugombezwa na wazazi wake kwa kukataa kuenda shule.

Joan Wekesa  ambaye alikuwa mwanafunzi katika shule ya upili ya Naburereya alijinyonga asubuhi ya Jumatatu akiwa ndani ya  nyumba ya mpenzi wake anayeishi karibu na soko ya Kabula.

Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na jamaa ambaye ni mjenzi katika mjengo unaoendelea katika eneo lile.

Wekesa alikuwa amemtembelea mpenziwe siku ya Jumapili na kulala kwake, jambo ambalo halikuridhisha mama yake aliyefika pale siku iliyofuata na kumwagiza aende shule.

Praxidese Wekesa  ambaye ni mama ya marehemu alisema kuwa juhudi zake za kujaribu kumshawishi bintiye akubali kuenda kusoma ziliangulia patupu na hapo akaamua kuenda kuita bwanake ili wasaidiane kumrejesha mtoto wao shule.

"Nilijaribu kuongea na yeye lakini hakuwa anaongea . Nilimuomba afungue mlango ili tuende naye nyumbani"  Bi Praxidese aliambia wanahabari.

Praxidese alisema kuwa bintiye alikuwa amekataa kabisa kurejea shuleni huku  akitishia kujinyonga iwapo angeendelea kukaripiwa ili arudi shuleni.

Alisema kwamba hakuamini Joan angetekeleza vitisho vyake vya kujinyonga na  kudai kuwa alishtuka sana aliporudi pale na kupata mwili wa mtoto wake ukining'inia kwenye kamba.