Hofu baada ya mwanamke kufariki ndani ya basi Mtito Andei

Hata hivyo bado haijabainika wazi kilichoangamiza mwanamke huyo.

Muhtasari

•Dereva wa basi hilo, Said Salim alikuwa amelisimamisha katika kituo hicho cha mafuta mida ya  saa kumi na mbili jioni walipogundua mwili wa marehemu.

•Kamanda wa polisi katika kaunti ya Makueni Joseph Ole Naipeyan amesema kuwa abiria wote walikuwa wametolewa nje na kutengwa pale kisha basi lile likafukizwa kwa dawa.

crime scene 1
crime scene 1

Habari na Patrick Nyakundi

Mwanamke mmoja aliaga dunia ndani ya basi lililokuwa linasafiri kutoka Mombasa kuelekea Nairobi jioni ya Jumanne.

Mwili wa mwanamke aliyetambulishwa kama Irene Nyambura ulipatikana ukiwa umelala kwa kiti cha basi aina ya Dreamline walipokuwa katika kituo cha mafuta maeneo ya Mtito Andei, kaunti ya Makueni.

Dereva wa basi hilo, Said Salim alikuwa amelisimamisha katika kituo hicho cha mafuta mida ya  saa kumi na mbili jioni walipogundua mwili wa marehemu.

Akithibitisha tukio hilo, kamanda wa polisi katika kaunti ya Makueni Joseph Ole Naipeyan alisema kuwa abiria wote walikuwa wametolewa nje na kutengwa pale kisha basi lile likafukizwa kwa dawa.

Hata hivyo bado haijabainika wazi kilichoangamiza mwanamke huyo.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Kibwezi huku upasuaji wa mwili ukisubiriwa kufanyika ili kubaini kilichosababisha maafa yale.