Hofu Busia baada ya mshukiwa wa mauaji kutoroka korokoroni

Mshukiwa anadaiwa kuhusika kwenye mauaji ya mmiliki wa hoteli ya Texas iliyo mjini Busia, Alfred Obayo

Muhtasari

•Wilson Simiyu 29, ambaye anatuhumiwa kuua mfanyibiashara mmoja mjini Busia anaripotiwa kutoroka mida ya asubuhi wakati seli yake ilipofunguliwa ili akachote maji.

•Inaaminika kuwa mshukiwa alipata majeraha alipokuwa katika harakati ya kutoroka kwani kulikuwa na kipande cha nyama ambacho kilikuwa kimekwama kwa chuma ya ukuta ule. Polisi wanaamini kuwa mshukiwa alitumia pikipiki kutoroka.

Jail bars
Jail bars
Image: FREEPIK

Polisi katika kaunti ya Busia wanawinda mshukiwa mmoja wa mauaji ambaye alitoroka alipokuwa amezuiliwa katika kituo cha polisi.

Wilson Simiyu 29, ambaye anatuhumiwa kuua mfanyibiashara mmoja mjini Busia anaripotiwa kutoroka mida ya asubuhi wakati seli yake ilipofunguliwa ili akachote maji.

Afisa mmoja wa polisi alimfungulia Simiyu ili akachote maji ya kuosha seli yake ila badala ya mshukiwa kuelekea kwa mfereji alipanda ukuta uliozunguka kituo hicho cha polisi na kuruka nje wakati afisa yule alikuwa anazungumza na mahabusu mwingine.

Inaaminika kuwa mshukiwa alipata majeraha alipokuwa katika harakati ya kutoroka kwani kulikuwa na kipande cha nyama ambacho kilikuwa kimekwama kwa chuma ya ukuta ule. Polisi wanaamini kuwa mshukiwa alitumia pikipiki kutoroka.

Simiyu alikuwa amehamishwa kutoka kituo cha polisi cha Kitale na kuzuiliwa katika kituo cha Busia  baada ya kukamatwa kwa tuhuma za makosa mengi ikiwemo wizi wa mabavu.

Alikuwa afikishwe mahakamani siku ya Jumatatu (Septemba 6) ili kusomewa mashtaka dhidi yake.

Mshukiwa anadaiwa kuhusika kwenye mauaji ya mmiliki wa hoteli ya Texas iliyo mjini Busia, Alfred Obayo.

Wakazi wametahadharishwa kuwa waangilifu na kupiga ripoti iwapo wana taarifa yoyote kuhusu aliko Simiyu.