Jamaa ajitoa uhai Embu na kuacha maelezo ya kufungua simu yake pamoja na namba ya siri ya Mpesa

Mwili wa Lawrence Munene 24, ambaye alikuwa fundi ulipatikana ndani ya chumba chake cha malazi siku ya Jumatatu.

Muhtasari

•Munene alikuwa ameandika ujumbe akiaga familia yake na kuomba msamaha kutoka kwa yeyote ambaye aliwahi kukosea.

•Familia ya marehemu ilisema kuwa waliweza kufungua simu yake ila hawakupata jumbe zoyote ambazo  ziliashiria sababu zake kujitoa uhai. 

meru
meru

Habari na Benjamin Nyaga

Hali ya mshtuko ilitanda katika kijiji cha Kithiruri, eneo la Kianjokoma, kaunti ya Embu baada ya jamaa mmoja kujitoa uhai na kuacha nambari yake ya siri ya Mpesa na kueleza jinsi ya kufungua simu yake.

Mwili wa Lawrence Munene 24, ambaye alikuwa fundi ulipatikana ndani ya chumba chake cha malazi siku ya Jumatatu.

Dada mdogo wa marehemu alienda kumgongea mlango mida ya saa tatu  ili aamke ila hakufunguliwa wa kupata jibu. Hapo akaarifu babake ambaye alivunja mlango wa chumba cha marehemu na kupata mwili wa mwanawe ukiwa umening'inia kando ya kitanda chake.

Munene alikuwa ameandika ujumbe akiaga familia yake na kuomba msamaha kutoka kwa yeyote ambaye aliwahi kukosea. Aliagiza kwamba mbuzi zake zikabidhiwe mtoto wa dadake.

"Naomba msamaha kwa yeyote ambaye nimekosea. Naomba muishi maisha mazuri na yenye furaha hadi tupatane tena. Nitawapeza sana" Ujumbe wa Munene ulisoma.

Siku ya Jumatano familia ya marehemu ilisema kuwa waliweza kufungua simu yake ila hawakupata jumbe zoyote ambazo  ziliashiria sababu zake kujitoa uhai.

Lawrence Munene 24, ambaye alijitoa uhai ndani ya nyumba yake Embu
Lawrence Munene 24, ambaye alijitoa uhai ndani ya nyumba yake Embu
Image: BENJAMIN NYAGA

Mama ya marehemu, Cecilia Wanja alisema kuwa mtoto wake alikuwa mpole, mnyenyekevu na mkarimu.

"Munene alikuwa mtoto mtulivu sana na alikuwa na uhusiano mzuri na kila mtu. Alisaidia kila alipohitajika kusaidia" Wanja alisema.

Wanja alisema kuwa mwanawe hakuonyesha dalili za shida yoyote na hakusema chochote cha kuashiria kuwa alikuwa na tatizo fulani, jambo ambalo linampa wasiwasi sana.

Mwili wa marehemu unahifadhiwa katika mochari ya Gakweroni.