Kijana mfugaji ashambuliwa na kuuawa na Simba Laikipia

Marehemu alikuwa ameandamana na takriban kondoo mia tatu.

Muhtasari

•Marehemu alikuwa safarini kupeleka kondoo wake malishoni katika kijiji jirani cha Endana kutoka Ilmotiok alipokumbana na kifo chake.

•Mwili wa Tereua Yiangale 18, ulipatikana  na mpita njia mida ya asubuhi karibu na eneo la Mlima Fisi.

Eneo la tukio
Eneo la tukio
Image: ELIUD WAITHAKA

Hali ya hofu ilitanda katika kijiji cha Lekiji, eneo la Laikipia Mashariki siku ya Alhamisi baada ya mfugaji mmoja kupatikana akiwa ameuawa na simba alipokuwa malishoni.

Mwili wa Tereua Yiangale 18, ulipatikana  na mpita njia mmoja mida ya asubuhi karibu na eneo la Mlima Fisi.

Kulingana na mwenyekiti wa Nyumba Kumi katika kijiji cha Lekiji Bw Resian Shembele, marehemu alikuwa safarini kupeleka kondoo wake malishoni katika kijiji jirani cha Endana akiwa ametoka Ilmotiok alipokumbana na kifo chake.

Ndugu ya marehemu ambaye pia ni chifu wa kijiji cha Ilmotiok ,Jacob Yiangele alisema kuwa kaka yake alishambuliwa mida ya saa kumi asubuhi. Marehemu alikuwa akiwalisha kondoo wake usiku kucha.

Yiangele alisema kuwa kwa wakati huo ndugu yake alikuwa ameandamana na takriban kondoo mia tatu.

Kulingana na afisa mkuu wa KWS katika eneo la Laikipia Rose Malenya, eneo kati ya ranchi ya Mpala na mbuga ya Oljogi ambapo mhasiriwa alishambuliwa panajulikana kuwa na wanyama pori.