Mshtuko Homabay baada ya mwanajeshi wa zamani kuua mamake kwa kisu kufuatia mgogoro wa shamba

Muhtasari

•Richard Odak ambaye alikuwa mwanajeshi nchini Tanzania anadaiwa kuua mamake Hellen Ajwang Odiango 91, nyumbani kwao katika eneo la Kamagak Magharibi, kaunti ndogo ya Kasipul

•Kufuatia  mgogoro huo Odak anaripotiwa kuondoka nyumbani kwao mwaka uliopita na kuenda mahali kusikojulikana kisha kurejea siku ya Ijumaa wiki iliyopita na kuanza kogombana na mamaye kama ilivyokuwa kawaida

Crime scene
Crime scene

Habari na Robert Omollo

Polisi katika kaunti ya Homabay wanasaka jamaa mmoja ambaye ni mwanajeshi wa zamani anayetuhumiwa kuua mamaye kufuatia mzozo wa shamba.

Richard Odak ambaye alikuwa mwanajeshi nchini Tanzania anadaiwa kuua mamake Hellen Ajwang Odiango 91, nyumbani kwao katika eneo la Kamagak Magharibi, kaunti ndogo ya Kasipul.

Inasemekana kuwa mshukiwa amekuwa akizozana na mamake kuhusu shamba hilo kwa kipindi kirefu. Odak amejenga nyumba yake pale.

Kufuatia  mgogoro huo Odak anaripotiwa kuondoka nyumbani kwao mwaka uliopita na kuenda mahali kusikojulikana kisha kurejea siku ya Ijumaa wiki iliyopita na kuanza kogombana na mamaye kama ilivyokuwa kawaida.

Inadaiwa kwamba wawili hao walizozana kwa kipindi kifupi kisha jamaa huyo kuchukua kisu na kumdunga mama yake kifuani na kwenye kichwa.

Baada ya hayo Bi Odiango alikimbizwa katika hospitali ya Rachuonyo Kusini ambako alifariki kutokana na majeraha mabaya ambayo alikuwa amepata mwilini.

Kamanda wa polisi katika eneo la Rachuonyo Kusini Lilies Wachira alisema kuwa mshukiwa alitoweka punde baada ya kutekeleza mauaji yale.

Uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo umeng'oa nanga huku juhudi za kumsaka mshukiwa ambaye alikuwa akiishi Tanzania zikiendelea.