Wazazi wa afisa Caroline Kangogo aliyedaiwa kujitoa uhai wakabidhi watoto wa marehemu kwa baba yao

Bwana Ng'eno ni afisa wa hadhi ya juu anayefanya kazi na kitengo cha polisi wa baharini, Mombasa.

Muhtasari

•Wazazi wa Kangogo wamekuwa wakiishi na wajukuu wao katika kijiji cha Nyawa kaunti ya Elgeyo Marakwet kwa kipindi cha miezi miwili ambacho kimepita.

•Kulingana na shangazi ya marehemu Kangogo, Bi Selinah Kibor, hatua ya kukabidhi watoto hao kwa Bw. Ngeno ilichukuliwa ili waweze kuungana tena na baba yao na pia waendelee na masomo.

Marehemu Caroline Kangogo
Marehemu Caroline Kangogo
Image: HISANI

Familia ya afisa Caroline Kangogo ambaye alidaiwa kujitoa uhai baada ya kutekeleza mauaji ya wanaume wawili miezi miwili iliyopita imekabidhi watoto wa marehemu kwa aliyekuwa bwanake.

Mzee Barnabas na mkewe Selinah Koriri walikabidhi wajukuu wao, mvulana wa miaka 11 na mseichana wa miaka 7, kwa baba yao Richard Ng'eno ambaye ametoka kaunti ya Kericho.

Bwana Ng'eno ni afisa wa hadhi ya juu anayefanya kazi na kitengo cha polisi wa baharini, Mombasa.

Wazazi wa Kangogo wamekuwa wakiishi na wajukuu wao katika kijiji cha Nyawa kaunti ya Elgeyo Marakwet kwa kipindi cha miezi miwili ambacho kimepita.

Kabla ya kufariki kwake, afisa Kangogo alikuwa ametoweka na kuacha watoto hao wawili nyumbani kwake mjini Nakuru  baada ya kuhusishwa na mauaji ya afisa  mwenzake John Ogweno.

Kangogo alikimbia eneo la tukio mjini  Nakuru na baadae kuhusishwa tena na mauaji ya mwanaume mwingine aliyetambulishwa kama Peter Ndwiga katika hoteli moja eneo la Kimbo, Kiambu.

Watoto wa Caroline Kangogo wakiwa pamoja na babu na nyanya yao wakati wa mazishi
Watoto wa Caroline Kangogo wakiwa pamoja na babu na nyanya yao wakati wa mazishi
Image: JESSICAH NYABOKE

Matukio hayo mawili ya kutishia yalifanya wazazi wa Kangogo kutuma binti yao mwingine aende Nakuru akachukue wajukuu wao ili wakae nao.

Kulingana na shangazi ya marehemu Kangogo, Bi Selinah Kibor, hatua ya kukabidhi watoto hao kwa Bw. Ngeno ilichukuliwa ili waweze kuungana tena na baba yao na pia waendelee na masomo.

"Tunaridhika kujua kwamba shemeji yetu ametafutia watoto hao shule nzuri ya bweni katika kaunti ya Kericho ambako wanasomea vizuri bila kusumbuliwa" Bi Kibor alisema.

Katika hafla ya mazishi ya aliyekuwa mkewe miezi miwili iliyopita, Bwana Ng'eno alikuwa ametulia na alikataa kuhutubia mamia ya waombolezaji ambao walikuwa wamejumuika.

Mwili wa Kangogo ulipatikana ndani ya bafu nyumbani kwa wazazi wake Elgeyo Marakwet na maafisa wa polisi wakasema kwamba alikuwa amejitoa uhai.

(Utafsiri: Samuel Maina)