Jamaa anayedaiwa kupiga mpenziwe risasi 5 kufuatia mzozo wa mapenzi Mukuru Kwa Njenga auawa na polisi

Muhtasari

•Joel alikuwa akiwindwa na polisi baada ya kuua mpenzi wake mwigizaji Monica Katee kwa kumpiga risasi tano kufuatia mzozo wa mapenzi.

•Usiku wa Ijumaa, Joel pamoja na mwenzake walipatwa na wapelelezi wakiwa wanapanga njama za kufanya mashambulizi katika mtaa wa Embakasi.

Monica Katee
Monica Katee
Image: HISANI

Jamaa anayedaiwa kuua mpenzi wake katika eneo la Mukuru Kwa Njenga mnamo Jumanne wiki iliyopita ni miongoni mwa washukiwa wawili wa ujambazi ambao walipigwa risasi na polisi usiku wa Ijumaa.

Joel alikuwa akiwindwa na polisi baada ya kuua mpenzi wake mwigizaji Monica Katee kwa kumpiga risasi tano kufuatia mzozo wa mapenzi.

Iliripotiwa kwamba  mnamo Septemba 14  mshukiwa alienda kwa nyumba ya Monica, wakazozana kwa kipindi kisha akampiga risasi tano kifuani na kwenye mgongo kabla ya kutoroka kwa kutumia pikipiki.

Iligunduliwa kuwa hapo awali Monica ambaye ni mwigizaji wa filamu za kienyeji alikuwa amepiga ripoti kwa polisi kuhusiana na vitisho ambavyo alikuwa amepewa na mpenziwe na tayari  polisi walikuwa wakimtafuta hata kabla ya kutekeleza unyama huo.

Usiku wa Ijumaa, Joel pamoja na mwenzake walipatwa na wapelelezi wakiwa wanapanga njama za kufanya mashambulizi katika mtaa wa Embakasi.

Joel alikuwa ameandamana na jamaa wengine wawili  wakati walikabiliwa na polisi na hapo wakaamua kukimbia kila mtu pande yake huku wakipiga risasi kuwaelekezea wapelelezi ambao walikuwa wakiwafuata.

Maafisa hao waliweza kuwaua wawili ikiwemo Joel huku mshukiwa wa tatu akiweza kutoroka na majeraha ya risasi mwilini.

Bosi wa polisi katika eneo la Embakasi John Nyamu alisema kwamba bastola moja na risasi 29 zilipatikana kufuatia operesheni hiyo.

Uchunguzi zaidi ulithibitisha kwamba bastola iliyopatikana na marehemu ilikuwa imetumika kutekeleza ujambazi katika maeneo tofauti  jijini Nairobi.