Hofu Nyeri baada ya mwili wa msichana aliyekuwa ametoweka kupatikana umetupwa ndani ya mto

Muhtasari

•Margret Waithera ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya Ngamwa aliripotiwa kutoweka  takriban wiki tatu zilizopita.

•Mwili wa msichana huyo uliashiria dalili kuwa alikuwa amebakwa kabla ya kuuawa na watu wasiojulikana.

Image: HISANI

Hali ya majonzi imetanda katika kijiji cha Mutonga eneo la Mukurweini, Nyeri baada ya mwili wa msichana wa miaka 13 kupatikana ukiwa umetupwa ndani ya mto Rwarai.

Margret Waithera ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya Ngamwa aliripotiwa kutoweka  takriban wiki tatu zilizopita.

Familia ya marehemu imekuwa ikimtafuta tangu atoweke bila mafanikio  na ndoto yao ya kupatanishwa tena na binti wao ilikatizwa baada yake kupatikana akiwa maiti.

Inaripotiwa kuwa mwili wa marehemu ulipatikana na wavuvi ukiwa umefungwa kwa gunia. 

Mwili wa msichana huyo uliashiria dalili kuwa alikuwa amebakwa kabla ya kuuawa na watu wasiojulikana.

Upelelezi zaidi kuhusiana na kisa hicho umeng'oa nanga huku familia ya marehemu ikianza mipango ya kumzika mpendwa wao.