Gari lililokuwa limebeba masista wa Katoliki lapatikana na mafurushi ya bangi, lita 35 za chang'aa

Muhtasari

•Inaripotiwa kuwa gari hilo lilikuwa na abiria watatu ambao ni masista wa kanisa la Katoliki ambao walikuwa wanaelekea kwa nyumba moja ya watawa iliyo katika mtaa wa Karen..

•Dereva alipoona kwamba hangeweza kuendelea kuwakimbia wapelelezi ambao walikuwa wamemwandama kweli aliamua kutoka kwa gari lake na kutoweka huku akiwaacha masista wale wakitetemeka kwa woga.

Image: TWITTER// DCI

Polisi wanazuilia gari moja ambalo lilipatikana likiwa limebeba mafurushi  13 ya bangi na lita 35 za vileo aina ya chang'aa.

Inaripotiwa kuwa gari hilo lilikuwa na abiria watatu ambao ni masista wa kanisa la Katoliki ambao walikuwa wanaelekea kwa nyumba moja ya watawa iliyo katika mtaa wa Karen..

Kulingana na DCI, wapelelezi kutoka kituo cha Langata walikuwa wamejaribu kusimamisha gari hilo lilipokuwa kwenye barabara ya Southern Bypass ila dereva akasita kusimama na kuongeza kasi ya gari .

Kufuatia hayo maafisa wale wakaingia kwenye gari lao aina ya Subaru na kukimbiza gari lile wakiwa na nia ya kubaini kwa nini lilikuwa limesita kusimama.

Masista wale walianza kufanya maombi ndani ya gari kufuatia mwendo wa kasi ambao dereva alikuwa anandesha gari lile ili kuepuka kukamatwa.

Dereva yule alipoona kwamba hangeweza kuendelea kuwakimbia wapelelezi ambao walikuwa wamemwandama kweli aliamua kutoka kwa gari lake na kutoweka huku akiwaacha masista wale wakitetemeka kwa woga.

Wapelelezi walichunguza kilichokuwa ndani ya gari lile na ndipo wakapata mafurushi ya bangi na chang'aa iliyokuwa imewekwa kwa mitungi.

Hata hivyo masista wale walijitenga mbali na mihadarati ile na kudai kwamba walikuwa wamemlipa dereva aliyetoweka ili awabebe kutoka Malaba hadi mtaa wa Karen.

Harakati za kumsaka mshukiwa zimeng'oa nanga huku gari husika likizuiliwa na maafisa wa DCI.