Moto uliosababishwa na wanajeshi wa Uingereza nchini Kenya haukuchunguzwa-Ripoti

Muhtasari

•Taasisi ya FOI imebainisha kuwa vikosi vya jeshi la Uingereza vilivyokuwa nchini Kenya vilisababisha matukio matano ya moto mwaka huu ambayo hayakuripotiwa.

Image: BATUK

Taasisi ya FOI imebainisha kuwa vikosi vya jeshi la Uingereza vilivyokuwa nchini Kenya vilisababisha matukio matano ya moto mwaka huu ambayo hayakuripotiwa, imeeleza tovuti ya Declassified UK, inayochambua habari za sera ya nje ya Uingereza.

Hatua hiyo imekuja siku kadhaa kabla ya Wizara ya Ulinzi ya Uingereza haijajiandaa kujitetea dhidi ya madai ya fidia yaliyotolewa na jamii katikati ya Kenya, ambayo yamesema vikosi vya Uingereza vilichoma ekari 12,000 za hifadhi ya wanyama pori kwa bahati mbaya wakati wa mazoezi mwezi Machi.

Mwanajeshi mmoja wa Uingereza anadaiwa aliandika ujumbe wa Snapchat kuhusu moto katika hifadhi ya Lolldaiga: "Miezi miwili nchini Kenya baadaye na tumebakiza siku nane tu. imekuwa vyema, tukasababisha moto, tukamuua tembo na tukajisikia vibaya lakini.....''

Tovuti hiyo imeorodhesha matukio yaliyopita ya moto karibu na Mlima Kenya kama ifuatavyo;

  • Tarehe 24 FebruarI: Moto uliwaka kwenye ranchi ya Ole Maisor eneo la mita 200 kwa 500 liliungua.
  • Tarehe 27 Februari: Moto uliwaka katika ranchi ya Mpala na kuunguza eneo la chini ya mita 200 kwa 200''.
  • Tarehe 28 Februari: Moto katika kituo cha Archers na kuunguza eneo la chini ya mita 200 kwa 200.
  • Tarehe 1 Machi: Moto katika eneo la Ol Doinyo Lemboro
  • Tarehe 1 Machi: Moto kwenye ranchi ya Ole Maisor

Hakuna tukio lolote la moto lililochunguzwa, tovuti hiyo imeeleza.

Imenukuu Wizara ya Ulinzi ikisema "ilihitajika tu kuchunguza moto mkubwa wakati upoteaji wa vifaa, majeruhi au uharibifu mkubwa wa mazingira umetokea".

"Hakuna nyaraka zilizoshikiliwa" kuhusu matukio mengine mawili ya moto ambayo Jeshi la Uingereza lilikiri kusababisha mnamo 2019, kwa sababu inasema "hawakufikia kiwango cha kufanyika uchunguzi".