"Alijiangusha mwenyewe ili kusabibisha vurugu" Idara ya polisi yawatetea maafisa wanaodaiwa kumshambulia Boniface Mwangi

Muhtasari

•Msemaji wa polisi Bruno Shioso amedai kuwa Mwangi alikuwa hatiani kwa kujaribu kuzuia maafisa ambao walikuwa wanatekeleza kazi yao kihalali.

•Kulingana na Shioso, Mwangi alionyesha uasi na kuzuia maafisa  kutekeleza kazi yao akiwa anakusudia kusaidia wakiukaji kuhepa kukamatwa ama kutishia maafisa wasiendeleze kazi yao.

•Shioso amewashukuru maafisa wa polisi na KRA waliohusika kwenye mvurugano huo kwa kuonyesha uvumilivu na utulivu licha ya kuzuiwa kufanya kazi yao na kuaibishwa hadharani.

Image: MAKTABA// BONIFACE MWANGI

Idara ya polisi imejitokeza kutetea wenzao ambao wanadaiwa kushambulia mwanaharakati mashuhuri Boniface Mwangi jijini Nairobi siku ya Ijumaa.

Kupitia ujumbe ambao ulitolewa siku ya Jumamosi, msemaji wa polisi Bruno Shioso amedai kuwa Mwangi alikuwa hatiani kwa kujaribu kuzuia maafisa ambao walikuwa wanatekeleza kazi yao kihalali.

Shioso amesema kwamba maafisa hao walikuwa wameandamana na maafisa wa KRA katika operesheni halali ya kuwakamata wafanyibiashara waliokuwa wamekwepa kulipa ushuru. 

"Mwanaharakati huyo alisisitiza kuitisha vitambulisho licha ya polisi kuwa wamevalia sare yao rasmi na kuwa wamebeba silaha zao rasmi. Operesheni hiyo ilifanyika mchana katika eneo wazi na tayari wakiukaji kadhaa walikuwa wamekamatwa na timu hiyo" Alisema Shioso.

Kulingana na Shioso, Mwangi alionyesha uasi na kuzuia maafisa  kutekeleza kazi yao akiwa anakusudia kusaidia wakiukaji kuhepa kukamatwa ama kutishia maafisa wasiendeleze kazi yao.

Uchunguzi wa polisi umebaini kuwa mwanaharakati huyo hakushambuliwa ila alijiangusha mwenyewe ili kusababisha vurugu ambazo zingepatia wakiukaji ambao walikuwa wamekamatwa nafasi ya kutoroka.

"Mwanaharakati huyo aliweza kutoroka kwenye eneo la tukio baada ya vurugu kutokea. Idara ya polisi inasikitishwa na tukio lisilofaa ambalo lilionyeshwa na camera likikusudia kusababisha mvutano kati ya polisi na raia"  Alisema Shioso.

Raia wameagizwa kuwachukulia maafisa wa polisi kama washirika wao ila sio maadui. Pia wameagizwa kushirikiana na polisi wanapokuwa wanatekeleza  kazi zao katika jamii na kusita kujaribu kuwazuia kwani hiyo ni hatia.

Kwenye video ambayo ilirekodiwa ikionyesha matukio ambayo yalitukia katika jumba la Pension Towers, Mwangi alioekana akikimbia huku maafisa watatu wa GSU walliokuwa wamejihami kwa bunduki na fimbo wakimfuata nyuma.

Baada ya kupiga hatua kadhaa mwanaharakati huyo alionekana akianguka chini na hapo maafisa ambao walikuwa wamemuandama wakamkamata na kumshambulia kwa viboko na mateke.

Msemaji wa polisi amewashukuru maafisa wa polisi na KRA waliohusika kwenye mvurugano huo kwa kuonyesha uvumilivu na utulivu licha ya kuzuiwa kufanya kazi yao na kuaibishwa hadharani.